choose language English English Swahili Swahili

Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Mh. Ummy Mwalimu leo tarehe 12-02-2019 amezindua huduma mpya ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa kutumia maabara maalum inayojulikana kwa jina la Cath-lab katika Hospitali ya Benjamin Mkapa iliyipo jijini Dodoma kwa lengo la kuboresha na kupanua wigo wa huduma za matibabu ya kibingwa nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa maabara hiyo, Waziri Ummy amesema kuwa kufunguliwa kwa maabara hiyo ni mafanikio makubwa kwa serikali katika kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi hivyo kupunguza idadi ya wagonjwa waliokuwa wakisafiri kwenda mbali kufuata huduma za matibabu.

“Huduma za kibingwa zimepunguza idadi ya wagonjwa waliokuwa wanasafiri au kupelekwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu kwa asilimia 95 kutokana na uboreshaji wa huduma za afya ndani ya nchi” amesema Waziri Ummy

Waziri Ummy amesema kuwa Serikali imekuwa ikiwajengea uwezo wataalam wa afya nchini ili waweze kutoa huduma bora kwa wananchi jambo ambalo limezaa matunda kwa kuwa wagonjwa wengi hivi sasa wanapata matibabu ndani ya nchi.

“Serikali yenu sikivu chini ya Mh.Rais Dkt. John Joseph Pombe Magufuli imeendelea kuboresha Sekta ya Afya kwa kuwasomesha na kuwajengea uwezo wataalam wetu na sasa matunda yake ndiyo haya, tulizowea kuona huduma kama hizi zinapoanzishwa lazima kuwe na wataalam kutoka nje ya nchi, lakini leo tunaona huduma imeanzishwa na wataalam wetu na hakuna mzungu hata mmoja” amesema.

Katika kuonesha furaha yake, Waziri Ummy ameupongeza uongozi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa na Taasisi ya Jakaya Kikwete kwa kuwa wabunifu na kushirikiana kutoa huduma bora za matibabu ya moyo kwa wananchi na kuzitaka hospitali na taasisi nyingine za afya kuiga mfano wao kwa lengo la kuboresha huduma za afya nchini.

“Nimefurahi kuona watalaam wetu mnashirikiana kujengeana uwezo na uzowefu, tulikuwa tunasema haya ndiyo makao makuu ya nchi, na kwa kuangalia uwekezaji mkubwa uliowekwa katika hospitali hii, nikawa najiuliza kwanini mambo hayaendi? Lakini ujio wa Dkt Chandika hapa BMH, umefanya mambo kwenda vizuri, wagonjwa wanakuja wengi na hata wabunge na viongozi mbalimbali wa serikali wanakuja kutibiwa hapa kwasababu wana imani na ubora wa huduma za hapa, nakupongeza sana wewe na timu yako” amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa Dkt. Alphonce Chandika akionekana mwenye furaha kupita kiasi amesema kuwa maabara hiyo iliyogharimu kiasi cha Tsh Bilioni 5 inatarajiwa kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo hivyo kupunguza adha ya wagonjwa kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za matibabu ambapo awali zilikuwa zikipatikana Dar Es Salaam kwenye Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete pamoja na Hospitali nyingine moja isiyo ya serikali.

“Tutaendelea kushirikiana na wataalam wenzetu kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ili kuweza kutoa huduma bora kwa wananchi na tunaiomba serikali kuongeza wataalam ili kuboresha zaidi upatikanaji wa huduma za afya” amesema.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi amesema kuwa hadi kufikia jioni jumla ya wagonjwa 13 kutoka Dodoma na mikoa ya jirani tayari walishakuwa wamefanyiwa uchunguzi katika maabara hiyo.

Aidha Prof. Janabi alitumia nafasi hiyo kuishukuru Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa kuwapa nafasi na heshima kubwa ya kushirikiana katika kutoa huduma za matibabu kwa wananchi.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Zainab Chaula amesema kuwa ipo haja ya kuwathamini madaktari wazalendo ambao wamekuwa wakijitoa kuokoa maisha ya watanzania. Dkt Chaula amesema kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika wataalam wa afya nchini ili kuweza kuwa na madaktari bingwa wengi wanaotoa huduma za kibingwa hapa hapa nchini pamoja na kuwekeza kwenye miundombinu na vifaa.

Mkurugenzi Mtendaji wa  Hospitali ya Benjamin Mkapa Dkt. Alphonce Chandika akisisitiza jambo kwenye halfa ya uzinduzi wa Maabara ya uchunguzi na tiba ya magonjwa ya Moyo.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akisalimiana na wananchi katika BMH Jijini Dodoma alipoenda kuzindua Maabara ya Uchunguzi na Tiba ya Magonjwa ya Moyo.

 

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (aliye mbele) akizindua rasmi maabara ya uchunguzi na tiba ya magonjwa ya moyo (Cathlab) katika Hospitali ya Benjamin Mkapa.

Imeandaliwa na
Kitengo cha Uhusiano.

CategoryNews

Copyright © 2020 - Benjamin Mkapa Hospital All rights reserved

Privacy Policy    |   Disclaimer   |    Sitemap   

English English Swahili Swahili