Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndungulile ameonesha kuridhishwa na huduma bora za afya zinazotolewa na Hospitali ya kibingwa ya Benjamin Mkapa.

Hayo yalibainishwa jana 28 Septemba, 2018 pale Naibu Waziri huyo alipofanya ziara ya kushitukiza katika Hospitali ya kibingwa ya Benjamin Mkapa iliyopo jijini Dodoma.

“Nipo kwenye ziara katika Hospitali ya Benjamin Mkapa ili kujionea hali ya huduma zinazotolewa katika hospitali hii na kwa kiasi kikubwa kwa kweli nimeridhishwa na maendeleo ya Hospitali na ubora wa huduma zinazotolewa hapa”.

Dkt. Ndungulile amebainisha sababu ya ziara yake kuwa ni katika kusimamia mikakati ya Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto ya kuhakikisha huduma za afya zinakuwa bora nchini kote na hasa Makao Makuu ya nchi ambapo serikali yote inaelekea kukamilisha utekelezaji wa kuhamia Dodoma.

“Dodoma sasa ni Makao Makuu ya nchi na sisi kama Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto tumedhamilia kuboresha huduma ili kuendana na mahitaji ya huduma za afya katika Makao Makuu ya nchi kwani sote tunajua kwamba serikali imehamia hapa, Bunge lilishakuwepo hapa hivyo, Dodoma kutakuwa na mahitaji makubwa sana ya huduma za afya, nimeanzia Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Dodoma na sasa nipo hapa ili kujihakikishia ubora wa huduma zetu za afya”.

Aidha, Dkt. Ndungulile ametoa wito kwa watanzania kufika katika Hospitali ya Benjamin Mkapa kwani ina vifaa vya kisasa na vinavyosaidia kutoa huduma bora lakini cha kushangaza vifaa hvyo vinahudumia watu wachache kuliko uwezo wake, mfano vifaa vinavyochunguza magonjwa ya saratani ya matiti, MRI, CT-Scan, nk vimekuwa vikitumika chini ya uwezo wake. Aidha, Hospitali ina miundo mbinu ya kisasa kama wodi mpya zenye uwezo wa kulaza wagonjwa zaidi ya 400, watumishi wenye sifa wakiwemo madaktari bingwa lakini bado wakuhudumiwa hawafiki kunufaika na uwekezaji huo mkubwa wa Serikali ya Awamu ya tano chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli.

“Nitoe rai hasa kwa wakazi wa Dodoma na mikoa jirani kwamba kuna huduma ambazo bado hatuzitumii vizuri. Tumekuwa tukiongelea masuala ya saratani ususani kwa kina mama, lakini pamoja na kuwa na mashine za kisasa za kubaini saratani ya matiti bado kinamama hawajitokezi kupata huduma hiyo matokeo yake mashine inahudumia watu 10 kwa wiki, wastani wa mtu mmoja kwa siku, jambo amabo linapunguza kasi ya kukabiliana na ugonjwa huu”.

Mheshimiwa  Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndungulile (kushoto) akinena jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa Dkt. Alphonce Chandika.

Mheshimiwa  Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndungulile (kushoto) akizungumza na mgonjwa aliyefika kupata matibabu katika hospitali ya Benjamin Mkapa.

Mheshimiwa  Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndungulile akitembelea miundombinu ya Hospitali ya Benjamin Mkapa.

Imeandaliwa na
Kitengo cha Uhusiano na Masoko.

Copyright © 2020 - Benjamin Mkapa Hospital All rights reserved

Privacy Policy    |   Disclaimer   |    Sitemap   

English English Swahili Swahili