Hospitali ya kibingwa ya Benjamin Mkapa iliyopo jijini Dodoma imetoa msaada wa kiti chenye magurudumu (wheelchair) kwa mtoto Christopher Elias Masaka mwenye umri wa miaka kumi akitokea kijiji cha Mtitaa wilayani Bahi jijini Dodoma aliyelazimika kukatwa miguu yake yote kutokana na maradhi yaliyomkabili kwa muda mrefu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa Dk. Alphonce Chandika amesema kwamba uongozi wa hospitali uliafikiana na kuona umuhimu wa kumpa faraja mtoto huyo kwa kumpatia matibabu bure pamoja na kumuwezesha kutembea kwa kutumia kiti hicho kilichonunuliwa kwa gharama za hospitali.

“jambo la kwanza na la lazima lilikuwa ni kuokoa maisha ya Christopher bila kujali uwezo duni wa familia yake lakini tusingeishia hapo kwasababu tayari mtoto ni muhitaji, hivyo, busara ilikuwa ni kumsaidia kupata urahisi wa kutembea kwa kiti hiki na sasa tunawaomba watanzania wamsaidie kupata miguu bandia, suala la elimu na mahitaji mengine muhimu ili aweze kukabiliana na maisha ya sasa na kutimiza ndoto zake”

Hata hivyo Dk. Chandika amesema,walifikia maamuzi ya pamoja kumpatia mtoto huyo kiti cha kutembelea (wheelchair) kwa kuwa wanatambua kuwa ni jukumu la kila mwanajamii kubeba mizigo ya watu wengine hasa wenye mahitaji maalum kama Christopher.

Kabla ya kukabidhi kiti hicho Naibu Waziri, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Mhe Anthony Mavunde mbele ya waandishi wa habari aliupongeza uongozi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuwahudumia watanzania kwa kutoa huduma za afya zilizo bora na kwa kutumia vifaa vya kisasa na hasa zoezi linaloendelea la upandikizaji wa figo pamoja na kuokoa maisha ya mtoto Christopher ambaye sasa ni mlemavu.

“Nakushukuru sana Mkurugenzi na uongozi mzima wa Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa kuamua kuonesha mfano kwa vitendo katika kuwasaidia watu wenye mahitaji maalum, halikuwa jukumu lenu kuafanya hili, lakini kwa moyo wenu wa kibinadam mkaona mfanye hili, nawashukuru sana”. Alisema Mavunde.

Mavunde aliongeza kwamba ni lazima jamii isimame mstari wa mbele katika kutoa huduma kwa watu wenye mahitaji maalum ikiwemo elimu na kusisitiza kuwa suala la jamii kujisahau na kudhani kwamba kuwasaidia wenye mahitaji maalum si jukumu lao au ni jukumu la serikali na familia husika linalopaswa kupingwa na badala yake elimu itolewe kwa uzito unaostahili ili jamii ijifunze kuwajibika kwa hali na mali kuwasaidia wahitaji na kufanikisha malengo yao.

“Na mimi kama binadamu lakini pia Naibu Waziri ninayehudumu Ofisi ya Waziri Mkuu baada ya kupata taarifa hii niliguswa sana lakini natamani kuona mtoto huyu anafikia malengo yake kielimu hivyo nimewaomba madaktari kutoka Dar es Salaam waje hapa kuchukua vipimo kwa ajili ya kumtengenezea Christopher miguu ya bandia ili kuunga mkono jitihada kubwa na nzuri zilizofanywa na hospitali hii, nina imani kwa kiasi fulani atafarijika japo nafahamu kwamba ni vigumu kuipokea hali hii kama ilivyo kwa mwanadamu yeyote. Pamoja na hilo, nitamfanya kuwa sehemu ya familia yangu ili niweze kumsaidia kwa karibu na kufuatilia maendeleo yake ikiwa ni pamoja na kumsomesha katika shule ya Fountain Gate Academy iliyopo Dodoma,” alisema Mavunde.

Mavunde aliwaasa na kuwaomba watanzania kuiga mfano wa Hospitali ya kibingwa ya Benjamin Mkapa ili kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania katika kutatua matatizo na kero za watanzania masikini na kuyaishi.

 

Imeandaliwa na

Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano

Copyright © 2020 - Benjamin Mkapa Hospital All rights reserved

Privacy Policy    |   Disclaimer   |    Sitemap   

English English Swahili Swahili