Hospitali ya kibingwa ya Benjamini Mkapa iliyopo jijini Dodoma imefanya upandikizaji wa figo kwa wagonjwa wengine watatu tarehe 27 na 28 mwezi wa nane 2018 kwa kushirikiana na madaktari bingwa kutoka Japan.Hii ni mara ya pili kwa Hospitali hii kufanya zoezi hili kubwa na lenye tija kwa taifa ambapo awali zoezi hili lilifanyika kwa mgonjwa mmoja mnamo mwezi machi mwaka huu.

Akiongea mbele ya waandishi wa Habari wakati wa kumkabidhi kiti cha kutembelea (wheelchair) mtoto mwenye ulemavu wa miguu Christopher Elias, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali Dkt. Alphonce Chandika alisema hii ni awamu ya pili kwa hospitali ya Benjamin Mkapa kufanya zoezi la kupandikiza figo.
“Hii ni mara ya pili tunafanya kazi hii kubwa na yenye tija kwa taifa ambapo awali tulifanikiwa kupandikiza figo kwa mgonjwa mmoja (Elias Sweti) mnamo mwezi machi mwaka huu 2018 ambaye ameshapona na anaendelea vizuri na shughuli zake za kawaida huku akihudhuria kliniki”
Aidha hospitali ya Benjamin Mkapa imefanya makubaliano na ‘Tokoshukai Medical Group’ ili kuwapeleka wataalam wa Hospitali ya Benjamin MKapa Japan kwa kipindi cha miezi sita ili wakaongeze uwezo katika eneo hili la upandikizaji figo kwa lengo la kuendelea kufanya huduma hii nchini bila kuwategemea wajapan.
“Zoezi hili ni endelevu na makubaliano yetu ni kwamba watakuwa wanakuja hapa kila baada ya miezi mitatu na tunategemea namba ya wagonjwa tutakaowapandikiza figo itaendelea kuongezeka, pia tumekubaliana kwamba tupeleke watalam wetu wawili nchini Japan wakaongeze uzowefu na ujuzi zaidi kwa kufanya kazi karibu na wajapani kwasababu wenzetu huduma hizi wanazifanya karibia kila siku”.

Aidha Dkt. Chandika aliwaasa wananchi kufanya uchunguzi wa mara kwa mara badala ya kusubiri figo kushindwa kufanya kazi kabisa ndo waende hospitali. Kwa kuchunguza afya mara kwa mara kunamuwezesha mtu kujua kama anatatizo kabla halijafikia hatua mbaya na kushindwa kutibika.
“ukifanya uchunguzi na kugundulika na tatizo la figo kabla haijapoteza uwezo wake wa kufanya kazi kunauwezekano wa kutibiwa na ukapona kabisa hivyo watanzania wenzangu tusisubiri mpaka tuugue na kuzidiwa kabisa”.

Kwa upande wake Naibu Waziri, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Mhe Anthony Mavunde mbele ya waandishi wa habari aliupongeza uongozi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa kuwa hospitali ya mfano jijini kutokana na kazi kubwa wanayoifanya ya kuwahudumia watanzania kwa kutoa huduma za afya zilizo bora hasa kwa zoezi linaloendelea la upandikizaji wa figo.
“Dodoma sasa ni Mkao Makuu ya nchi na moja kati ya masuala muhimu ni afya, na Hospitali ya Benjamin Mkapa mmedhihirisha kwamba mna uwezo wa kuhudumia wananchi wote na hivi sasa mmepiga hatua na kuwa hoispitali ya mfano hasa katika zoezi hili la kupandikiza figo jambo ambalo sisi kama serikali tunaliunga mkono na mnavyozidi kupata uzowefu, hatutapeleka tena wagonjwa nje ya nchi kwani wote watakuja kupata huduma hiyo hapa katika Hospitali yenu hivyo tutapunguza matumizi makubwa ya fedha kupeleka wagonjwa nje ya nchi”.
Zipo njia nyingi za kulinda figo isishambuliwe na maradhi nazo ni ni pamoja na kunywa maji ya kutosha. Kuwepo na maji ya kutosha mwilini kunaifanya figo ichuje vizuri uchafu ikiwemo vimelea kwenye mfumo wa ukojoaji na kuzuia utengenezwaji wa mawe kwenye figo; kuwa na uwiano kati ya uzito na urefu (body mass index) kutokuwa uwiano mzuri kati ya uzito na urefu hukaribisha magonjwa kama sukari, shinikizo la juu la damu na magonjwa haya ni adui mkubwa wa figo. Njia yingine ni kutumia dawa sawasawa na maelekezo ya daktari, kumekuwepo na kasumba ya watu kujitibu wenyewe na kusahau kwamba dawa ni sumu inayoweza kuumiza figo na mfumo mzima wa mwili wa mwanadamu. Watu wanaaswa kulinda afya zao kwa kufanya uchunguzi wa mara kwa mara.
Imeandaliwa na
Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano

Copyright © 2020 - Benjamin Mkapa Hospital All rights reserved

Privacy Policy    |   Disclaimer   |    Sitemap   

English English Swahili Swahili