Dkt. Gwajima ameyasema hayo wakati akizindua rasmi kitabu cha huduma kwa Mteja, pamoja na Idara ya magonjwa ya saratani na maabara ya patholojia na kufurahishwa na mafanikio makubwa ya Hospitali hiyo.

Awali akisoma taarifa yake wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi  Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa Dkt. Alphonce Chandika  alibainisha kuwa  Mkataba huo wa huduma kwa mteja unaelezea kwa undani haki na wajibu wa mteja/mgonja pamoja na mtoa huduma na kwamba Hospitali ina njia mbalimbali za kupokea maoni hayo  na kuyashughulikia kwa wakati.

“Tuna kituo cha kupokea maoni na malalamiko, tuna kifaa cha kielektroniki (Customer feedback system) cha kukusanya maoni  ambacho kinamhitaji mteja kubonyeza kitufe kutoa maoni yake, na pia tumeteua mtumishi mmoja anayepita sehemu za kutolea huduma na kuongea na wananchi kujua malalamiko yao, na Menejimenti imeweka mikakati ya kutatua malalamiko hayo” alisema Dkt. Chandika.

Katika hotuba yake, Mhe. Gwajima  amesifu jitihada zilizofanywa na uongozi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa ya kuanzisha huduma ya matibabu ya saratani  pamoja na maabara ya patholojia na kueleza kuwa Hospitali ya Bejamin Mkapa imekuwa ikijiongeza kwa  kuanzisha huduma ambazo ni muhimu kwa wananchi .

Ameongeza kuwa kwa muda mrefu wakazi wa Kanda ya kati hawakuwa na sehemu ya kupata matibabu ya saratani na iliwalazimu wananchi hao kusafiri  umbali mrefu kufuata matibabu, hivyo kuanzishwa kwa huduma hizi kutaleta nafuu kwa wakazi wa Kanda ya Kati.

 “Matibabu haya ya Saratani hapa nchini yanatolewa katika hospitali za Ocean Road na Muhimbili za Dar es Salaam, Bugando ya Mwanza, KCMC ya Kilimanjaro, Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mkoa wa Mbeya na Hospitali nyingine binafsi. Ukiangalia Taasisi ambazo zinatoa matibabu haya ya saratani zote ziko pembezoni mwa nchi yetu. Eneo la Kati ya nchi, Mkoa wa Dodoma na mikoa jirani ya Iringa, Morogoro, Singida, Tabora na Kigoma kwa muda mrefu ilikosa huduma za matibabu haya ya saratani” alisema Dkt. Gwajima.

 Aidha Dkt. Gwajima ameeleza kuwa  Saratani kama moja ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza inashika nafasi ya tano kwa wanaume na ya pili kwa wanawake kwa kusababisha vifo vitokanavyo na magonjwa yasiyo ya kuambukiza nchini huku zaidi ya 75% ya wagonjwa wa Saratani hufika katika Vituo vya Matibabu wakiwa wamechelewa sana na kuwawia vigumu madaktari kutibu na kuponya ugonjwa huo.

Dkt. Gwajima amewataka wananchi kujenga tabia ya kupima afya zao mara kwa mara ili wakibainika kuwa wana shida waanze tiba mapema kwani saratani inatibika ikiwahiwa.

Copyright © 2020 - Benjamin Mkapa Hospital All rights reserved

Privacy Policy    |   Disclaimer   |    Sitemap   

English English Swahili Swahili