BMH YAPELEKA HUDUMA ZA KIBOBEZI ZA MATIBABU YA MOYO KWA WATOTO NA WATU WAZIMA MKOANI TABORA KATIKA HOSPITALI YA RUFAA YA NKINGA
Na Jeremia Mwakyoma
Igunga, Tabora - Dec 27, 2025
Timu ya Madaktari Bingwa Wabobezi wa Moyo kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) wamepiga kambi Mkoani Tabora Wilaya ya Igunga katika Hospitali ya Rufaa ya Nkinga wakitoa huduma za Uchunguzi na Matibabu ya Moyo kwa watoto na Watu Wazima.
Dkt. Emiliana Myovela kutoka Kurugenzi ya Utafiti, Mafunzo, Huduma Mkoba na Mashirikiano ya Kimataifa ya BMH akimuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji amesema kuwa huduma katika kambi hiyo zimeanza kutolewa leo na zitakwenda hadi Novemba 28, 2025 na kupitia kambi hizo za matibabu BMH inapeleka huduma za Ubobezi za Uchunguzi, Matibabu na Elimu kwenye Mikoa na Wilaya mbalimbali hapa nchini.
"Serikali imeona umuhimu wa kufikisha huduma za Ubobezi karibu na Wananchi kwenye Mikoa na Wilaya wanazoishi hivyo kuwapunguzia gharama na kuwapa urahisi wa kupata huduma. Katika kambi hi hapa Hospitali ya Nkinga tunaendelea kuwajengea uwezo na kubadilishana uzoefu na Madaktari wa Nkinga" alisisitiza Dr Emiliana.
Aidha, amemshukuru Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Serikali yake kuwekeza na kufanya mageuzi katika Sekta ya Afya kwa upande wa miundombinu, Vifaa tiba, madawa na kuendeleza Wataalamu katika Ubobezi jambo linalowezesha huduma kuwafikia Wananchi.
Nae Daktari Bingwa Mbobezi wa Magonjwa ya Moyo kwa Watoto kutoka BMH Mwanaisha Getrude Seugendo amesema katika kambi hiyo wamewafanyia uchunguzi Wananchi na kuweza kubaini baadhi yao wana changamoto za moyo bila wao wenyewe kujua hali zao na hivyo kuwaanzishia matibabu.
"Pia tumeweza kuwabadilishia matibabu Wagonjwa ambao wamekuwa wakitumia dawa kwa muda mrefu kwa kununua kutoka maduka ya dawa bila kufanya vipimo kujua maendeleo ya hali zao" alisisitiza Dkt. Seugendo
Aidha, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Nkinga Dkt. Juma Nahonyo amebainisha kuwa wamepokea Wananchi kutoka Mkoa wa Tabora na Mikoa ya jirani kama Shinyanga na Katavi waliokuja kupata vipimo na matibabu katika kambi hiyo na kuendelea kutoa wito zaidi kwa Wananchi kuja kufanya uchunguzi wa magonjwa ya moyo.
"Tunashukuru kambi inayoendelea inasaidia Wataalamu wa Hospitali yetu ya Nkinga wamepata fursa ya kujengewa uwezo kupitia Madaktari Bingwa Wabobezi wa BMH, pia mwitikio wa Wananchi umeonesha wanazihitaji huduma, kwa kutumia ushirikiano uliopo baina yetu Hospiti ya Nkinga na BMH, tunafikiria uwezekano wa kuandaa kambi hizi mara kwa mara kulingana na mahitaji" alisisitiza Dkt. Nahonyo.
Kwa upande wake Bi. Sophia Mfumia Mtaalamu Mbobevu wa Vifaa tiba vya Magonjwa ya Moyo kutoka kampuni ya KAS Medics wasambazaji wa vifaa hivyo na madawa amesema kampuni yao wameamua kuungana na BMH kutoa mchango wao ili kuwezesha Madaktari Bingwa kwenda Tabora Hospitali ya Nkinga sambamba na madawa na vifaa tiba katika kambi hiyo.