Mafunzo na Huduma Mkoba
Published on June 27, 2025

Sehemu ya Mafunzo na Uhamasishaji Jamii katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) ni kitovu muhimu cha ujenzi wa uwezo, maendeleo ya kitaaluma, na ushirikiano na jamii. Ilianzishwa kwa kuzingatia dira ya hospitali ya kutoa huduma maalum na za kibingwa katika afya ya kinga, tiba, utafiti, ubunifu na mafunzo kwa kutumia teknolojia mpya, ikiwa na lengo la kuboresha utoaji wa huduma za afya nchini Tanzania.
Sehemu hii ina jukumu la kipekee katika nyanja mbili: ndani ya hospitali, inaratibu na kuwezesha mafunzo kwa watumishi, wanafunzi wa vitendo, madaktari wabobezi wa vitendo, na mafunzo endelevu ya kitaaluma (CME); na nje ya hospitali, inaongoza juhudi za kutoa huduma kwa jamii kwa kuwalenga wananchi walioko maeneo ya mbali au wasiofikiwa kwa urahisi, kupitia huduma za kinga, uchunguzi, tiba, na elimu ya afya. Kupitia ushirikiano na taasisi za elimu, serikali, na wadau wa maendeleo kutoka ndani na nje ya nchi, sehemu hii inahakikisha BMH inaendelea kuwa kinara katika mafunzo ya vitendo na afya ya jamii nchini Tanzania.
Aidha, sehemu hii ni kichocheo cha kuimarisha mifumo ya afya kupitia programu zilizopangwa vyema zikiwemo: uongozi wa kitaaluma, msaada wa kitaalamu kwa hospitali za mikoa na wilaya, na usambazaji wa mbinu bora za utoaji huduma. Kwa kuimarisha uwezo wa watumishi wa afya na kukuza uelewa wa jamii kuhusu masuala muhimu ya afya, sehemu hii inachangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha dira ya hospitali ya kuwa “Hospitali ya kisasa inayotegemea sayansi mpya kwa jamii yenye afya bora na maendeleo endelevu ya taifa.”
Huduma Zinazotolewa na Sehemu
- Uratibu wa Mafunzo kwa Vitendo na Mafunzo ya Kliniki
Sehemu hii inaratibu na kusimamia mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi wa fani mbalimbali za afya kama tiba, uuguzi, na taaluma shirikishi za afya kwa ajili ya kupata uzoefu wa kazi katika mazingira halisi ya hospitali. - Mafunzo Endelevu ya Kitaaluma (CPD)
Kwa kushirikiana na wadau wa ndani na nje, sehemu hii hutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa ajili ya kuboresha maarifa, ujuzi, na utendaji kazi wa watumishi wa afya, hivyo kuboresha utoaji wa huduma. - Msaada wa Kitaalamu kwa Vituo vya Afya
Hutoa msaada wa kitaalamu na kujenga uwezo kwa hospitali za mikoa na wilaya katika kuboresha ubora wa huduma za afya. - Programu za Uhamasishaji Jamii
Hutoa huduma kupitia kliniki tembezi na uhamasishaji wa afya kwa jamii, ikilenga uchunguzi wa afya, kinga dhidi ya magonjwa, na utoaji wa matibabu katika kampeni za elimu ya afya. - Mafunzo ya Ufundi (Vocational Training)
Sehemu hii inaratibu mafunzo mafupi ya vyeti katika fani zifuatazo:
- Vyeti vya Umahiri katika:
ü Ultrasound ya Msingi
ü Uendeshaji wa Huduma za Upasuaji (Operating Theatre Management)
ü Tiba za Dharura, Wagonjwa Mahututi na Majeruhi (Emergency, Critical Care, and Trauma)
ü Huduma za Figo na Dialysis
ü Anesthesia (kuanzia miezi 3 hadi mwaka 1)
- Stashahada ya Kawaida katika Radiografia ya Utambuzi (Diagnostic Radiography – miaka 3)
Watumishi na Utaalamu
Ufanisi wa sehemu hii unategemea timu ya wataalamu wa kada mbalimbali wanaofanya kazi kwa kushirikiana kulingana na majukumu ya sehemu hii:
- Waalimu wa Sayansi za Afya
Ni wakufunzi waliobobea katika fani za Radiografia, Uuguzi, Famasi, Lishe ya Kliniki, Tiba, Figo na Anesthesia. Wanaendesha programu za kitaaluma. - Walezi na Wasimamizi wa Mafunzo ya Vitendo
Ni madaktari bingwa, wataalamu na wakufunzi kutoka idara mbalimbali wanaotoa mafunzo kwa vitendo, usimamizi na ushauri kwa wanafunzi. - Wataalamu wa Kliniki na Afya ya Jamii
Hushirikiana kutekeleza shughuli za afya ya jamii, kampeni za uchunguzi, na elimu ya afya kwa jamii. - Waratibu wa Mafunzo na Programu
Husimamia ushirikiano na wadau, kupanga mafunzo, kuratibu CPD na shughuli zote za mafunzo ya vitendo na huduma za jamii. - Watendaji wa Utawala na Usaidizi
Hushughulikia shughuli za kila siku, usimamizi wa taarifa, mawasiliano, na kuratibu shughuli kati ya hospitali na wadau.
Miundombinu na Teknolojia
- Majengo na Vifaa
Sehemu hii ina ofisi mbili, maabara ya kompyuta yenye vifaa mbalimbali vya TEHAMA, maabara za kisasa kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo na mafunzo kwa njia ya kuiga (simulation), pamoja na kumbi za mafunzo zinazoweza kuchukua hadi wanafunzi 150 kwa wakati mmoja.
Mafanikio na Hatua Muhimu
- Kuendeleza mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi kutoka taasisi mbalimbali za mafunzo
- Kuanzisha kozi mpya fupi mwaka 2025 zenye lengo la kuimarisha umahiri wa watumishi wa afya, zikiwemo:
ü Cheti cha Umahiri katika Uendeshaji wa Huduma za Upasuaji
ü Cheti cha Umahiri katika Tiba ya Dharura, Wagonjwa Mahututi na Majeruhi
ü Cheti cha Umahiri katika Dialysis na Huduma za Figo
- Kuanzisha ushirikiano wa kimataifa na wadau kutoka Japan, Italia, Kuwait, Uholanzi, Ujerumani, Kanada, Australia, na Marekani kwa lengo la kubadilishana ujuzi na rasilimali.
Mipango ya Baadaye
- Upanuzi wa Programu za Mafunzo: Kupanua idadi ya stashahada kutoka programu moja ya Radiografia hadi kujumuisha fani nyingine kama Udaktari wa Meno, Optometria, na Fiziotherapia
- Kuimarisha Ushirikiano: Kujenga na kuimarisha ushirikiano na wadau wa ndani na nje kwa ajili ya kuendeleza uwezo wa hospitali na kuboresha ubora wa huduma za afya
- Kuongeza Huduma za Jamii: Kupanua huduma za uhamasishaji na uchunguzi wa afya kwa jamii hususan katika maeneo ya pembezoni na yasiyofikika kwa urahisi
- Kuanzisha Programu za Mabadilishano: Kuanza mpango wa mabadilishano ya kitaaluma kati ya BMH na taasisi nyingine za ndani na kimataifa kwa lengo la kubadilishana maarifa na ujuzi