Mwanzo / Kurasa / Magonjwa ya dharula, Usingizi & Chumba cha Mahututi

Magonjwa ya dharula, Usingizi & Chumba cha Mahututi

Published on June 30, 2025

Article cover image

Hospitali ya Benjamin Mkapa ni mojawapo ya taasisi muhimu za afya nchini Tanzania, hasa katika utoaji wa huduma za matibabu ya dharura. Idara ya Tiba ya Dharura inahakikisha kuwa wagonjwa wanaohitaji huduma za haraka wanapata matibabu kwa wakati na kwa ufanisi. Ripoti hii inaangazia historia ya kuanzishwa kwa idara, utendaji wake, mafanikio, uwekezaji wa serikali, rasilimali watu, mafunzo, mahitaji ya vifaa na watumishi, mapendekezo ya kuboresha huduma, na mipango ya baadae.


MWAKA WA KUANZISHWA

Idara ya Tiba ya Dharura katika Hospitali ya Benjamin Mkapa ilianzishwa mwaka 2019 kama sehemu ya juhudi za kuboresha huduma za afya kwa wakazi wa Dodoma na Kanda ya Kati. Lengo kuu lilikuwa ni kupunguza vifo na ulemavu unaotokana na kuchelewa kupata huduma za dharura.


UTENDAJI WA IDARA

Tangu kuanzishwa kwake, idara imeshahudumia zaidi ya wagonjwa 400,000 waliokumbwa na hali mbalimbali kama vile:

  • Ajali za barabarani

  • Kifafa cha shinikizo la damu

  • Mshituko wa moyo (heart attack)

  • Kiharusi (stroke)

  • Magonjwa ya mfumo wa upumuaji (pumu, nimonia)

  • Maambukizi makali (sepsis)

Kumekuwa na ongezeko la wagonjwa kila mwaka kutokana na uelewa mkubwa wa jamii na upanuzi wa huduma za hospitali.


MAFANIKIO MAKUU

Idara imepata mafanikio yafuatayo:

  • Kuboresha huduma za dharura kupitia matumizi ya vifaa vya kisasa kama vile mashine za kupumulia (ventilators), ultrasound ya mkononi (point-of-care), na X-ray inayobebeka.

  • Kuweka mfumo madhubuti wa rufaa kwa kushirikiana na vituo vya afya vya mikoa kupitia simu ya dharura.

  • Mafunzo endelevu kwa madaktari na wauguzi katika huduma za dharura, yakifadhiliwa na mdau aliyesaidia ujenzi wa kituo cha mafunzo ya vitendo.

  • Ushirikiano na taasisi za ndani na nje ya nchi kama Abbott Fund Tanzania, Emergency Medical Association of Tanzania (EMAT), na TiKA.

  • Ushiriki katika kukabiliana na majanga kama moto wa Morogoro na maporomoko ya ardhi Katesh, Manyara.

  • Kutoa mafunzo ya dharura katika hospitali zote za mikoa na wilaya tatu za Kanda ya Kati.

  • Kutoa huduma za afya kwa watoto 720 kupitia kambi ya matibabu katika Shule ya Msingi Ihumwa na Kituo cha Kulelea Yatima Kikombo.

  • Kuanza awamu ya mwanzo ya huduma za dharura kwa Jiji la Dodoma kwa kushirikiana na wadau.

  • Kutekeleza miongozo ya kukabiliana na majanga ndani na nje ya hospitali.


UWEKEZAJI WA SERIKALI

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeisaidia idara kwa:

  • Kununua vifaa vya kisasa vya uchunguzi na matibabu.

  • Kujenga miundombinu ya kisasa ya Idara ya Tiba ya Dharura.

  • Kuajiri watumishi waliobobea katika huduma za dharura.

  • Kutoa bajeti ya uendeshaji kila mwaka kwa ajili ya huduma za dharura.


MAHITAJI YA VIFAA NA RASILIMALI WATU

Ili kuboresha utoaji wa huduma, idara inahitaji kwa haraka:

  • Jengo la kisasa lenye vitengo vya uokoaji (resuscitation), uangalizi (observation), wagonjwa wa nje, na watoto.

  • Mashine 4 za kupumulia kwa wagonjwa mahututi.

  • Mashine 2 za ECG na mashine 1 ya ultrasound.

  • Vitanda 40 maalum vya huduma ya dharura na ICU.

  • Kuongezwa kwa madaktari na wauguzi wa dharura.

  • Ambulansi zenye vifaa vya kisasa kwa ajili ya majanga na huduma za dharura za BMH.


RASILIMALI WATU WALIOPO KWENYE IDARA

Kwa sasa idara inajumuisha:

  • Daktari Bingwa wa Tiba ya Dharura 1

  • Madaktari wa Tiba 16

  • Wauguzi Waliandikishwa 18

  • Wahudumu wa Afya 13


MAFUNZO NA UBORESHAJI WA UJUZI

Hospitali, kwa kushirikiana na wadau wake, hutoa mafunzo ya mara kwa mara kuhusu:

  • Huduma ya kwanza na matibabu ya dharura

  • Matumizi ya vifaa vya kisasa vya uchunguzi na matibabu

  • Mbinu za kuokoa maisha ya wagonjwa mahututi

  • Usimamizi wa afya wakati wa majanga na dharura


MAPENDEKEZO YA KUBORESHA HUDUMA KUFIKIA VIWANGO VYA TAIFA NA KIMATAIFA

Ili kuimarisha uwezo wa idara na kufikia viwango vya kimataifa, yafuatayo yanapendekezwa:

  • Kuongeza bajeti ya idara ili kufanikisha upatikanaji wa rasilimali na wafanyakazi wa kutosha.

  • Kuimarisha ushirikiano na taasisi za kimataifa kwa ajili ya misaada ya kifedha na mafunzo.

  • Kuanzisha programu maalum za mafunzo ya tiba ya dharura kwa wahudumu wa afya.

  • Kuongeza idadi ya vitanda vya huduma ya dharura.

  • Kuboreshwa kwa mifumo ya kidijitali kwa ajili ya ufuatiliaji wa mgonjwa kwa wakati halisi na utunzaji wa kumbukumbu.

  • Kuimarisha mfumo wa rufaa wa ndani na wa kimataifa.

  • Kupata magari ya wagonjwa yenye vifaa vya hali ya juu kwa huduma za kabla ya hospitali (pre-hospital care).


MIPANGO YA BAADAYE

Kwa ajili ya kuendelea kuboresha huduma za dharura, hospitali inapanga:

  • Kuajiri watumishi zaidi wa tiba ya dharura waliobobea.

  • Kununua vifaa vya kisasa zaidi kwa uchunguzi na matibabu.

  • Kutoa elimu kwa umma kuhusu huduma za dharura na msaada wa kwanza.

  • Kuanzisha mfumo wa kukabiliana na majanga kwa Jiji la Dodoma, kutokana na umuhimu wake kitaifa na ongezeko la watu na maendeleo.


HITIMISHO

Idara ya Tiba ya Dharura ya Hospitali ya Benjamin Mkapa ni nguzo muhimu katika utoaji wa huduma za afya kwa wakazi wa Dodoma na Kanda ya Kati. Licha ya changamoto zilizopo, msaada endelevu kutoka kwa serikali, uongozi wa hospitali, na wadau mbalimbali unaendelea kuimarisha utoaji wa huduma za dharura na kupunguza vifo na madhara yanayotokana na hali za dharura za kiafya.