Sehemu ya Saratani na Tiba ya Nyuklia
Published on August 12, 2022

Idara ya Saratani katika Hospitali ya Benjamin Mkapa ilianzishwa mwaka 2018 kwa lengo la kutoa huduma maalum kwa wagonjwa waliogundulika kuwa na saratani. Ilianza ikiwa na daktari mmoja bingwa wa saratani (oncologist), na imepanuka kwa haraka ili kutoa huduma mbalimbali kama vile ushauri wa kitaalamu, tiba ya kemikali (chemotherapy), huduma za kupunguza maumivu (palliative care), pamoja na huduma za kinga kama uchunguzi wa saratani na elimu ya afya kwa jamii. Ingawa huduma za mionzi (radiotherapy) bado hazijaanza kutolewa, ujenzi wa kitengo cha kisasa cha tiba ya mionzi unaendelea, na unatarajiwa kuboresha zaidi huduma za saratani mara utakapokamilika.
Huduma Zitolewazo na Idara ya Saratani
- Ushauri wa Kitaalamu: Tunatoa huduma za ushauri kwa ajili ya uchunguzi, kuweka hatua za ugonjwa (staging), na kupanga mpango maalum wa matibabu kwa kila mgonjwa.
- Tiba ya Kemikali (Chemotherapy): Matibabu ya chemotherapy hutolewa kulingana na aina ya saratani aliyonayo mgonjwa, huku tukifuatilia kwa karibu ili kuhakikisha matokeo bora.
- Huduma za Kupunguza Maumivu (Palliative Care): Kwa wagonjwa wenye saratani iliyo katika hatua ya juu au wasioweza kupona, tunatoa huduma ya kupunguza maumivu, kudhibiti dalili, na kuboresha ubora wa maisha.
- Huduma za Kinga:
ü Uchunguzi wa Saratani: Tunafanya uchunguzi wa saratani za kawaida kama saratani ya matiti, shingo ya kizazi, na tezi dume kwa lengo la kugundua mapema na kutoa tiba kwa wakati.
ü Elimu ya Afya: Tunatoa elimu kwa umma kuhusu njia za kuzuia saratani, visababishi vyake, na umuhimu wa uchunguzi wa mapema.
Huduma za Kinga na Ushirikiano na Jamii
- Programu za Uchunguzi wa Saratani: Idara inafanya uchunguzi wa mara kwa mara wa saratani ya matiti, shingo ya kizazi, na tezi dume.
- Elimu kwa Jamii: Tunaendesha programu za kufikisha elimu kuhusu kinga ya saratani, mtindo bora wa maisha, na umuhimu wa uchunguzi wa mara kwa mara kupitia warsha, semina, na kampeni za afya.
- Kampeni kwa Umma: Idara hushiriki kikamilifu katika kampeni za uhamasishaji kwenye shule, maeneo ya kazi, na jamii kwa ujumla.
Wataalamu na Rasilimali Watu
- Daktari Bingwa wa Saratani (Oncologist): Anasimamia mpango wa matibabu ya wagonjwa na mwelekeo wa huduma katika idara.
- Daktari wa Tiba ya Jumla: Husaidia kusimamia huduma za kila siku za wagonjwa na kuhakikisha huduma kamilifu.
- Wauguzi: Wauguzi wanne waliopata mafunzo ya oncology wanahudumia moja kwa moja wagonjwa wa saratani, kutoa elimu na msaada kwa familia.
- Wafamasia: Kuna mfamasia mmoja bingwa wa tiba za saratani na mafamasia watano wa kawaida wanaosaidia katika utoaji wa dawa na ushauri.
- Ushirikiano wa Kisekta: Idara hushirikiana na wataalamu wa ustawi wa jamii, lishe, saikolojia, na tiba ya viungo kutoa huduma ya kina na inayozingatia mahitaji ya mgonjwa.
Miundombinu na Teknolojia
- Miundombinu ya Kisasa: Idara ina maeneo ya kisasa ya kutolea chemotherapy na huduma za palliative care, yaliyojengwa kwa kuzingatia faragha na ustawi wa mgonjwa.
- Kitengo cha Mionzi (Kinachojengwa): Kitengo kipya cha tiba ya mionzi kinajengwa na kitakapokamilika, kitawezesha matibabu ya saratani kwa njia ya mionzi kwa usahihi zaidi.
Mafanikio na Hatua Muhimu
- Idadi ya Wagonjwa: Idara hutibu takribani wagonjwa 5,000 wa saratani kila mwaka.
- Upanuzi wa Huduma: Mbali na chemotherapy na ushauri, huduma za palliative care na elimu kwa jamii zimeanzishwa.
- Ujenzi wa Kitengo cha Mionzi: Hii ni hatua muhimu kuelekea utoaji wa huduma kamilifu za saratani.
Mikakati na Malengo ya Baadaye
- Kituo Bora cha Saratani: Kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), tunalenga kuanzisha kituo bora cha saratani kitakachotoa huduma za uchunguzi, matibabu na utafiti kwa kiwango cha juu.
- Upanuzi wa Huduma: Kuanzisha tiba mpya kama immunotherapy na targeted therapies ili kutoa matibabu yenye ufanisi zaidi na madhara kidogo.
- Upasuaji wa Saratani (Surgical Oncology): Kuongeza wataalamu wa upasuaji wa saratani kwa ajili ya kutoa huduma kamili ya tiba.
- Kukamilisha Kitengo cha Mionzi: Kukamilika kwa kitengo cha mionzi kutaboresha zaidi matibabu ya wagonjwa wa saratani.
- Kuongeza Elimu kwa Jamii: Kupanua kampeni za elimu na uchunguzi hadi kufikia maeneo ya pembezoni.
- Maendeleo ya Wafanyakazi: Kuwekeza katika mafunzo ya mara kwa mara kwa wataalamu wetu ili kuhakikisha wanabaki na ujuzi wa kisasa.
Kwa taarifa zaidi au kupanga miadi, tafadhali wasiliana nasi kupitia namba:
📞 +255 735 000 002