KIKAO CHA WATUMISHI WOTE-KIPAUMBELE CHA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA MWAKA HUU MPYA WA FEDHA NI KUBORESHA ZAIDI UTOAJI HUDUMA ZA AFYA
Published on July 09, 2025

Na Jeremia Mwakyoma.
Picha Jeremiah Mbwambo na Carine Senguji
DODOMA – JULAI 9, 2025
Uongozi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) umesema kuwa kipaumbele cha kwanza cha Hospitali hiyo katika mwaka huu mpya wa fedha wa 2025/2026 ni kueendelea kutoa huduma bora zaidi za Afya kwa Wananchi.
Mkurugenzi Mtendaji wa BMH Prof. Abel Makubi amesema hayo wakati akizungumza na watumishi wote wa Hospitali hiyo katika kikao cha pamoja cha Uongozi wa BMH na Watumishi ambapo msisitizo mkubwa ulikuwa kuendelea kuboresha zaidi huduma zinazotolewa na BMH kwa Wananchi.
“Tukiwa tumeanza mwaka mpya wa fedha wa Serikali, watumishi wote wa BMH tutambue kipaumbele chetu cha kwanza ni kuendelea kuboresha zaidi utoaji huduma za Afya kwa wananchi, hicho ni kipaumbele cha kwanza cha Serikali katika Sekta ya Afya, Serikali imeboresha upande wa miundombinu, upatikanaji madawa, vifaa tiba na watumishi hivyo jukumu letu sisi watumishi ni kuongeza kutoa huduma bora zaidi za Afya kwa wananchi” alisisitiza Prof. Makubi.
Prof. Makubi aliongeza kuwa watumishi wote wa BMH wanatakiwa kuwajibika kwa matokeo katika kuwahudumia wananchi na kuzingatia nidhamu ya kazi na kuwataka watumishi hao kuwa na “sense of ownership” katika kutekeleza majukumu yao na kutoa muda wao kuwasaidia wananchi. Aidha, aliishukuru Serikali kwa kuendelea kuiwezesha Hospitali ya BMH kuwekeza miundombinu na huduma mbalimbali.
“Tumeanzisha huduma mpya ya Klinic ya Wateja Maalum, Wateja wa Kimataifa na Uchunguzi wa Kina wa Afya wa Kibingwa (Royal, International Patients and Master Health Check up Clinic) ambayo itazinduliwa Julai 10, 2025 na Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama, jukumu letu watumishi ni kuwa tayari kuhudumia kliniki hiyo kulingana na viwango vinavyotakiwa kwenye kliniki hiyo” alisisitiza Prof. Makubi.
Aliongeza kuwa baadhi ya miradi inayolenga kuboresha huduma za BMH ambayo michakato yake ipo katika hatua mbalimbali ni pamoja na kuanzisha kliniki mpya na ya kisasa itakayokuwa katikati ya Jiji la Dodoma (eneo la mjini), Kituo cha Umahiri cha matibabu ya magonjwa ya Saratani ambacho ujenzi wake umefikia asilimia 59%, Kituo cha Umahiri cha Upandikizaji Figo kwa kushirikiana na taasisi ya TOKOSHUKAI ya nchini Japan, Kituo cha Umahiri cha matibabu ya Figo na hivi karibuni tumepata mradi wa Kituo cha Umahiri cha Upandikizaji Uloto na Magonjwa ya Damu cha Afrika Mashariki.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uuguzi wa BMH Mwanaidi Makao amebainisha kuwa ziara waliyoifanya timu ya Wataalamu wa BMH kwenye Hospitali kubwa Jijini Dar es salaam imesaidia kujifunza uzoefu mpya wa kuhudumia wateja kwa viwango vya ubora, kuboresha miundombinu, mifumo, usimamizi na uendeshaji lakini imeonesha BMH inayo fursa kubwa ya kuongeza huduma zake kutokana na mazingira mazuri yaliyopo BMH na tayari maboresho mbalimbali yameshaanza.
Nae Mkurugenzi wa Huduma Shirikishi wa BMH Dkt. Humphrey Sawira amesema upatikanaji wa dawa kwa wagonjwa wanaotibiwa BMH ni wa kuridhisha kwa sasa umefikia asilimia kati ya 97 na 98 huku upande wa muda wa wagonjwa kusubiria dawa umepungua na sasa mgonjwa anasubiria kwa dakika 15 hadi 30 tu.