KAMBI YA MADAKTARI BINGWA WA MOYO KUTOKA BMH YAHITIMISHWA MKOANI RUVUMA, WAGONJWA WA MOYO ZAIDI YA 120 WANUFAIKA

Published: Dec 10, 2025
KAMBI YA MADAKTARI BINGWA WA MOYO KUTOKA BMH YAHITIMISHWA MKOANI RUVUMA, WAGONJWA WA MOYO ZAIDI YA 120 WANUFAIKA cover image
Na Jeremia Mwakyoma
SONGEA - RUVUMA, NOV. 21, 2025 
 
Kambi ya Madaktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kwa Watoto na Watu wazima kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) yahitimishwa Mjini Songea Mkoani Ruvuma  huku zaidi ya Wagonjwa wa Moyo 120 wakiwa wamenufaika na huduma za uchunguzi, matibabu na elimu ya magonjwa ya moyo. 
 
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo na Huduma Mkoba wa BMH Rahyan Mbisso aliyeongoza timu kutoka BMH amesema kuwa kiwango kizuri cha mwitikio wa Wananchi kwenye kambi hiyo iliyofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma imeonesha uhitaji mkubwa wa huduma za kibingwa na kibobezi kwa Wananchi. 
 
"Wananchi wamejitokeza kwa wingi kuja kupata huduma katika kambi hii na wengi wameomba kambi hizi zifanyike mara kwa mara na kuwa na Wataalamu wengi zaidi na sisi kama Hospitali tutakwenda kuliwekea Mkakati wa kuandaa zaidi kambi hizi kulingana na mahitaji" aliongeza Ndg. Mbisso. 
 
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Songea, Dkt. Magafu Majura, amesema pamoja na mwitikio wa Wananchi, kambi imekuwa na manufaa kwa madaktari na wauguzi wa hospitali hiyo kupitia ushirikiano na madaktari kutoka BMH kupata nafasi ya kujengewa uwezo na kuongeza ujuzi.
 
 
Aidha, Dkt. Majura amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha sekta ya afya kupitia uboreshaji miundombinu, upatikanaji vifaa tiba na ajira kwa watumishi 
 
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Moyo kwa Watoto Mwanaisha Serugendo kutoka BMH amewaasa wananchi kuzingatia ushauri wa kitaalamu kuhusu namna ya kujikinga na magonjwa ya moyo na amewataka Wataalamu kuendelea na utoaji elimu wa Magonjwa hayo kwa Wananchi ili kukuza uelewa katika Jamii.