Waziri wa afya azitaka hospitali za kanda na taasisi zinazotoa matibabu kuiga mfano wa BMH.
Published on July 11, 2025

Na; Carine Senguji na Gladys Lukondo, DODOMA. JULAI 10 2025.
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama ( Mb), amezitaka Hospitali za Kanda na taasisi zinazohusika na kutoa matibabu kuiga mfano wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) na kuanzisha kliniki ya Wateja Maalum, Wateja wa Kimataifa na Uchunguzi wa afya wa kina wa Kibingwa.
Mhe. Jenista ametoa wito huo mapema hii leo alipokuwa akizindua kliniki hiyo katika Hospitali ya Benjamin Mkapa ambapo amepongeza kuwa Kliniki hiyo ni ya ubora wa viwango vya juu ambavyo Wateja wa kutoka nje wanapenda mazingira ya Kliniki hiyo.
"Wito wangu kwa vituo vyote vya kutolea huduma za afya kikanda na taasisi zinazotoa huduma za afya tuanzishe huduma hii ambayo imeanza hapa BMH inayosaidia kuongeza Wateja wa kutoka nje ya nchi katika huduma za tiba utalii na hata Wateja wa ndani itasaidia kupunguza msongamano kwa wananchi wanaotaka kupata huduma za haraka," amesema Mhe. Jenista.
Mhe. Jenista ameendelea kuwataka watumishi wa umma na sekta binafsi ambao wanaenda kufanya uchunguzi wa afya zao nje ya nchi hawqna haja ya kwenda nje badala yake wafike BMH kwa huduma bora za aina hiyo.
"Hapa ni makao makuu ya nchi na kuna taasisi nyingi za umma na binafsi naomba nitoe wito kwenu kufanya uchunguzi wa afya zenu BMH kwani ina uwezo mkubwa na serikali imefanya uwekezaji wa kutosha katika hospitali hii lakini pia BMH mnaweza kuingia makubaliano na taasisi hizi kwa ajili ya kuwapatia huduma hizo," ameongeza Mhe. Jenista.
Mhe. Jenista amewapongeza madaktari kwa kujitoa kwao kuwahudumia wananchi mida ambayo sio masaa ya kazi.
"Niwapongeze madaktari nimeona hapo mtakuwepo saa kumi na moja asubuhi na mtaingia pia baada ya mida ya kazi kuanzia saa kumi na mbili jioni mpaka saa nne," ameeleza Mhe. Jenista.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Prof. Abel Makubi ameomba miongozo za tiba utalii kukamilika kwa mapema ili ianze kutumika mapema.
"Mhe. Waziri tunaomba miongozo hii ya tiba utalii kukamilika mapema ili ianze kutumika na sisi kama wasaidizi wako tunaahidi kukupa ushirikiano kwenye suala hili la tiba utalii," amesema Prof. Makubi.