WANANCHI 648 WA WILAYA YA CHEMBA WANUFAIKA NA HUDUMA ZA MADAKTARI BINGWA WA MACHO, MASIKIO, PUA NA KOO KWA USHIRIKIANO WA BMH, UDOM NA CBM
Published on May 26, 2025

Na; Carine Senguji, Mei 24 2025. CHEMBA
Jumla wananchi 648 wamenufaika na kambi ya madaktari bingwa wa macho, masikio, pua na koo iliyofanyika wilaya ya Chemba kwa ushirikiano wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na shirika la Christian Blind Mission (CBM).
Daktari bingwa wa magonjwa ya macho, Jacinta Feksi amesema kuwa wananchi wa wilaya hiyo ya Chemba wamenufaika na huduma za upasuaji wa macho na wengine wamenufaika na huduma za uchunguzi na matibabu ya macho, masikio, pua na koo.
"Wananchi 131 wamenufaika na huduma za upasuaji wa macho na wengine 517 wamenufaika na huduma za uchunguzi na matibabu ya macho, masikio, pua na koo kwenye kambi tuliofanya wilayani hapa," amesema Dkt. Jacinta.
Dkt. Jacinta ameendelea kwa kuainisha magonjwa ambayo wananchi wengi wa wilaya ya Chemba walikua wakisumbuliwa nayo.
"Katika upande wa macho tumepata wagonjwa wengi wa mtoto wa jicho, pressure ya macho na allergy ya macho na kwenye upande wa masikio watu wengi walikua wakisumbuliwa na usaa kwenye masikio ambayo hupelekea kuathiri usikivu," ameongeza dkt. Jacinta.
Bi. Zuhura Shabani ambae ni mkazi wa kijiji cha Mlogia ameshukuru ujio wa madaktari bingwa wilayani chemba.
"Nashukuru ujio wa madaktari hawa kutoka BMH na UDOM kwani kwa kipindi cha miaka miwili nilikua sioni kabisa kutokana na tatizo la mtoto wa jicho ila baada ya upasuaji niliofanyiwa naweza kuona vizuri kabisa hivyo nashauri hata wale wenzangu wanaoogopa kujitokeza kwenye kambi kama hizi waje ili kupata matibabu ya uhakika," amesema Bi. Zuhura.
Kambi hii ushirikiano kati ya BMH, UDOM na CBM ambapo ilianza Mei 19 2025 na kutamatika Mei 23 2025.