MENEJIMENTI YA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA (BMH) YATOA MKONO WA SIKUKUU KWA WATUMISHI WAKE

Published: Dec 23, 2025
MENEJIMENTI YA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA (BMH) YATOA MKONO WA SIKUKUU KWA WATUMISHI WAKE cover image

●Mkurugenzi Mtendaji Prof. Abel Makubi awashukuru Watumishi wa BMH kwa Utendaji mzuri katika mwaka 2025, awataka kuongeza uwajibikaji na ubora wa huduma katika mwaka 2026. 

 

Na Jeremia Mwakyoma

DODOMA - DISEMBA 23, 2025 

 

Akikabidhi zawadi hizo, Prof. Makubi amewataka Watumishi wote wa BMH kutambua kuwa uongozi unatambua mchango wao katika kuwahudumia wananchi na kuwasisitiza kuzidi kujipanga katika kuwajibika zaidi na kuboresha zaidi ubora wa huduma ili kufikia malengo yaliyowekwa kwa mwaka 2026. 

 

"Kwa ushirikiano kati ya Menejimenti na Watumishi tumeweza kufika zaidi ya asilimia 90% katika utekelezaji wa majukumu yetu kwa kipindi cha miezi hii 6  inayokamilika mwezi huu Disemba 2025, hivyo miezi 6 ijayo kuanzia Januari 2026 tunahitaji kuongeza tija zaidi ya utendaji kulingana na malengo tuliyojiwekea" alisisitiza Prof. Makubi. 

 

Aidha, Prof. Makubi aliongeza kuwa Menejimenti  ya BMH siku zote ipo pamoja na Watumishi wake na inatambua mchango wao mkubwa hivyo imeona ni vema kuwapa watumishi mkono wa  shukrani kwa kuwapa zawadi za sikukuu, huku akiwataka  Wakuu wa Idara zote za BMH kuongeza usimamizi kwa kutambua wao ndio injini ya Usimamizi wa utendaji kazi na utoaji Huduma bora na kuwataka Watumishi wote  kwa pamoja kuboresha utendaji, utoaji huduma bora, kuimarisha mawasiliano na wagonjwa na kushughulikia malalamiko machache yatakayojitokeza. 

 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu wa BMH Bw. Teophory Mbilinyi amesema kuwa kurugenzi yake itaendelea kusimamia utendaji wa Watumishi kuhakimisha tija iliyokusudiwa inafikiwa, itaendelea kushauri namna bora zaidi ya kutambua kazi nzuri na mchango wa Watumishi kupitia motisha ili kuwaongezea watumishi ari zaidi na morali ya kazi. 

 

Nae Mkurugenzi wa Uuguzi wa BMH Bi. Mwanaidi Makao ameelezea kuwa, kitendo alichokifanya Mkurugenzi Mtendaji kuwapa watumishi mkono wa sikukuu  kinaonesha namna anavyowathamini watumishi wote, inaonesha umoja na mshikamo kati ya uongozi na Watumishi wote, itawaongezea  watumishi ari ya kujituma zaidi, ubunifu na jitihada zaidi katika kazi. 

 

Akiwawakilisha watumishi wa BMH, Mratibu wa maoni na ubora wa huduma Bw. Bahati Sayi amesema kuwa mkono wa zawadi ya sikukuu ambayo watumishi wa BMH wamepokea kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji unawakumbusha kuboresha zaidi uwajibikaji wao kwa kuwapa wananchi huduma bora za matibabu, kwa wakati na kwa kuzingatia miongozo ya nchi katika kutoa huduma za Afya kwa wananchi.