HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA KUANZISHA FURSA ZA USHIRIKIANO WA KIMKAKATI NA TAASISI YA KOREA FOUNDATION FOR INTERNATIONAL HEALTHCARE (KOFIH)
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), Prof. Abel Makubi, amefanya mazungumzo ya kimkakati na Bi. Hyunkyung Kim, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa wa Taasisi ya Korea Foundation for International Healthcare (KOFIH), kuhusu fursa za kuimarisha ushirikiano katika sekta ya afya.
Mazungumzo hayo yalijikita katika maeneo ya mafunzo ya tiba za kibingwa, uhamishaji wa teknolojia na ujuzi, uboreshaji wa ubora wa huduma za afya na usalama wa wagonjwa, usimamizi wa hospitali pamoja na kujenga uwezo wa watumishi, kwa lengo la kuimarisha utoaji wa huduma za afya na kuboresha matokeo ya matibabu kwa wagonjwa.
Mkutano huo, uliowezeshwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Jamhuri ya Korea, umefanyika pembezoni mwa Mkutano wa Kimataifa wa Shirikisho la Hospitali Duniani (International Hospital Federation – IHF) wa mwaka 2026, uliofanyika Seoul, Korea Kusini.
Ushirikiano huo ni hatua muhimu katika azma ya Hospitali ya Benjamin Mkapa kuwa miongoni mwa Vituo Bora vya Umahiri katika utoaji wa huduma za afya za kibingwa na kibingwa bobezi.
