HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA KWA KUSHIRIKIANA NA MADAKTARI BINGWA KUTOKA NCHINI UTURUKI WAENDESHA MAFUNZO YA KIBOBEZI YA UPASUAJI MASIKIO

Published: Dec 05, 2025
HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA KWA KUSHIRIKIANA NA MADAKTARI BINGWA KUTOKA NCHINI UTURUKI WAENDESHA MAFUNZO YA KIBOBEZI YA UPASUAJI MASIKIO cover image

Na  Jeremia Mwakyoma

DODOMA - DISEMBA 2, 2025

 

Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kwa kushirikiana na Shirika la Hands Giving Lives la nchini Uturuki kupitia timu ya Madaktari Bingwa Wabobezi wa Masikio Pua na Koo kutoka nchini Uturuki, yametolewa kwa Madaktari Bingwa Wabobezi wa BMH, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Madaktari Bingwa kutoka Hospitali za Rufaa za Mikoa ya Dodoma, Tabora na Manyara.

 

Akizungumza wakati wa Mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Upasuaji wa BMH Dkt. Henry Humba akimuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, amesema kuwa BMH ina jukumu la kuzijengea uwezo Hospitali za Rufaa za Mikoa ya Kanda ya Kati na Mikoa ya Jirani na kupitia mafunzo hayo yaliyoandaliwa kwa ushirikiano wa pande hizo mbili, yanasaidia kutekeleza jukumu hilo la kuzijengea uwezo Hospitali hizo.

 

"Mafunzo yameendeshwa kwa namna bora kabisa, yamekuwa ya vitendo zaidi ya nadharia kwa kutumia maabara maalumu ya mafunzo (Skills Lab) ambayo ina vifaa vya bandia vya kufundishia na kujifunzia, mazingira yaliandaliwa yanayofanana na vyumba vya Upasuaji ili kuwapa madaktari ujuzi na uzoefu halisi kama wanavyokuwa wakiwafanyia Wagonjwa upasuaji" amesisitiza Dkt. Humba.

 

Dkt. Humba amemshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali ya awamu ya sita kwa mashirikiano mazuri na Serikali ya Uturuki na kusema kuwa mafunzo yataleta manufaa makubwa kwa kuzingatia  kuwa Dodoma na Mikoa inayozunguka kuna Wagonjwa wengi wenye Changamoto za kusikia ambao wanahitaji vipandikizi vya usikuvu (Cochlear implants), kutokwa usaha  Masikioni na wengine wanaopata ajali na mishipa ya fahamu kubanwa  (Facial Nerve Paralysis).

 

Kwa upande wake Rais wa Shirika la Hands Giving Lives na kiongozi wa Timu ya Madaktari Bingwa kutoka Uturuki Bi. Hatice Ozdemir amebainisha kuwa ujio wao katika Hospitali ya Benjamin Mkapa mbali na kutoa mafunzo kuwaongezea Madaktari Bingwa Ujuzi na Uzoefu lakini watajikita katika kutoa matibabu kwa Wagonjwa wenye kuhitaji msaada wa kweli wa matibabu na hususani wale wasio na uwezo.

 

Ameongeza kuwa kwa kipindi kirefu shirika lake na Timu ya Madaktari Bingwa wametembea nchi mbalimbali na wamejifunza jambo moja la muhimu linalohitajika ni mafunzo  kuwajengea Uwezo Wataalamu wazawa na kubadilishana nao uzoefu huku akishukuru ushirikiano uliopo baina ya nchi za Tanzania na Uturuki.

 

 Aidha, Washiriki wa Mafunzo hayo hususani kutoka Hospitali za Rufaa za Mikoa ya Dodoma, Tabora na Manyara wamekiri kuwa katika Mikoa yao kuna Wahitaji wengi wa huduma za matibabu ya Kibingwa ya Masikio hususani Upasuaji wa Masikio unaosababishwa na matatizo mbalimbali hivyo mafunzo hayo yataongeza uwezo wa kuwahudumia Wananchi.

 

Mkuu wa Idara ya Masikio pua na Koo wa BMH Dkt. Faustine Bukanu amesema kuwa baada ya mafunzo hayo, timu za madaktari Bingwa wa BMH na kutoka Uturuki wataendelea kutoa matibabu kwa Wagonjwa ikiwemo kuwafanyia Upasuaji wa Masikio wale wote watakaohitaji matibabu hayo na kubainisha kambi hiyo ya pamoja ya matibabu itakamilika Disemba 7, 2025.