HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA YAKUTANA NA WAHARIRI WA VYOMBO VYA HABARI , KUELEKEA KILELE CHA MAADHIMISHO YA MIAKA 10 , TAREHE 15 JULAI 2026

Published: Jul 04, 2026
HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA YAKUTANA NA WAHARIRI WA VYOMBO VYA HABARI , KUELEKEA KILELE CHA MAADHIMISHO YA MIAKA 10 , TAREHE 15 JULAI 2026 cover image
  • ·       Wazungumzia mafanikio ya miaka 10 ya BMH
  • ·       Wito wa Wadau kushiriki katika mfuko wa matibabu ya upandikizaji Figo na  uloto kwa watoto wenye Sickle Cell

 

 

Na. Jeremiah Mbwambo, Dar es Salaam, 21 Mei 2026



Mkurugenzi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Profesa Abel Makubi amesema katika kuelekea  kilele cha Maadhimisho ya Miaka 10 tarehe 15 Julai 2026 , Hospitali hiyo  kwa kushirikiana na Mfuko wa Bima ya Afya wanaendelea kushirikisha wadau wenye moyo wa kutoa kwa lengo la kuwezesha zaidi ya shilingi bilioni saba ndani ya miaka miwili ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika kusaidia matibabu ya wagonjwa wanaohitaji huduma za upandikizaji wa Figo na Uloto.



Prof. Makubi amesema hayo Mei 21, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa Semina  kwa Wahariri wa Vyombo vya Habari ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka kumi tangu kuanzishwa kwa hospitali hiyo.



Amesema licha ya hatua kubwa ya iliyofikiwa na hospitali hiyo katika kutoa huduma za kibingwa na bobezi bado idadi ya wagonjwa wanaohitaji huduma za Figo na Uloto zimeendelea kuongezeka nchini.



“Katika kuelekea  Maadhimisho ya miaka kumi ya hospitali yetu, tumeona ni muhimu kuanzisha utamaduni wa wadau nchini wenye moyo wa kutoa na kuguswa na mahitaji ya Wananchi wenzao katika kuunga mkono juhudi za Serikali ambazo zimeleta Mapinduzi makubwa ya huduma za kibingwa na kibobezi, amesema Prof. Makubi.



Ambapo amewaomba wananchi, taasisi na mashirika mbalimbali yatakayoguswa yaweze kuchangia Mfuko huo ili kuokoa maisha ya Watanzania wanaosumbuliwa na ugonjwa wa Figo na Selimundu (Sickle cell) kwa kutuma michango yao kwenda akaunti namba 102501000407 (BOT) Jina BMH organ Transplant  au kutumia kumbukumbu namba 986930000001 Jina BMH organ Transpant.



Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Damu na Upandikizaji Uroto wa Hospitali hiyo, Stella Malangahe amesema uwepo wa mfuko huo utaongeza uelewa kwa jamii kuhusu umuhimu wa uchangiaji wa viungo pamoja na matibabu ya magonjwa ya figo, huku akisisitiza haja ya wananchi kujitokeza mapema kupima afya zao ili kuepuka madhara makubwa yanayosababishwa na magonjwa hayo.



Naye, Daktari Bingwa wa Upasuaji na  Upandikizaji Figo wa  Hospitali hiyo,  Prof. Masumbuko Mwashambwa amesema kuwa maadhimisho hayo ya miaka kumi ya hospitali hiyo ya Benjamin Mkapa yataambatana na shughuli mbalimbali ikiwemo utoaji wa elimu kwa umma, kampeni za uchangiaji wa Mfuko huo maalum na kuonesha mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya afya tangu kuanzishwa kwa hospitali hiyo.