HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA YATOA MATIBABU YA UBINGWA BOBEZI WA MAGONJWA YA NGOZI KWA WANANCHI WILAYANI KONDOA
Na Jeremia Mwakyoma
KONDOA - JUNI 24, 2026
Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) imeweka kambi ya siku mbili Wilayani Kondoa ikitoa huduma ya uchunguzi na matibabu ya kibobezi ya magonjwa ya ngozi kwa wananchi wa Wilaya ya Kondoa na Wilaya nyingine za jirani.
Akizungumza katika kambi hiyo inayoendelea kufanyika katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Kondoa, Daktari wa Ngozi na magonjwa ya zinaa kutoka BMH Kahabi Kimotoli amesema kuwa wameshughulikia changamoto zote za ngozi na zinaa, pumu ya ngozi, magonjwa ya nywele na kucha huku mwitikio wa Wananchi ukiwa wa kuridhisha.
"Ndani ya muda mfupi tumewapa huduma zaidi ya wagonjwa 50 na wengine zaidi wanaendelea kujitokeza, hii imekuwa fursa nzuri kwa wananchi ambao wameshindwa kufika BMH Dodoma, huduma za uchunguzi na dawa za kutibu zimewafikia hapa Kondoa na tumetumia nafasi hii kuwajengea uwezo watoa huduma za Afya katika Hospitali ya Kondoa" alisisitiza Dkt. Kimotoli
Nae Petro Alex Mteknolojia Dawa kutoka BMH amesema katika kambi hiyo, wameleta Dawa ambazo hazipatikani sokoni zinatengenezwa na BMH kupitia Wataalamu wake wabobezi na Mashine za teknolojia za kisasa zinazosaidia wagonjwa wenye kuhitaji dawa zenye mchanganyiko maalumu ambazo zimepunguzwa viambata vyenye athari kwa mwili wa binadamu lakini zenye uwezo mkubwa wa kutibu magonjwa ya ngozi.
Akitoa maoni ya Wananchi wa Kondoa Bi. Angel Raphael amesema kuwa ujio wa Madaktari wa BMH umewapunguzia adha, muda na gharama za kuwafata Wataalamu hao mjini Dodoma, ameshukuru pamoja na matibabu waliyopata lakini wamepewa elimu ya kutosha juu ya magonjwa ya ngozi na utunzaji wa ngozi huku akiomba kambi hizo ziwe za mara kwa mara.