BMH NA UDOM WAIWEZESHA BUGANDO KUPANDIKIZA FIGO KWA MARA YA KWANZA

Published: Apr 24, 2026
BMH NA UDOM WAIWEZESHA BUGANDO KUPANDIKIZA FIGO KWA MARA YA KWANZA cover image

18 April 2026

 

Jopo la Wataalamu 12 (Madaktari Bingwa, wauguzi, usingizi na ganzi) kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) wameweza kuwajengea uwezo Watalaamu Mabingwa wa Hospitali ya Kanda Bugando mjini Mwanza na kushirikiana ambapo kwa pamoja wamempandikiza figo mgonjwa wa kwanza katika hospitali hiyo.

 

Upasuaji huo wa mafanikio umefanyika kwa mgonjwa mwenye umri wa miaka 40 (Mwanaume),mkazi wa Mkoa wa Mwanza, kwa ushirikiano wa karibu kati ya wataalamu hao.

 

Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Bugando Sr. Dr. Alicia Massenga ametoa shukrani kwa BMH na UDOM.

 

"Tunawashukuru sana wenzetu kutoka BMH kupitia Mkurugenzi wa Hospitali ya Benjamini Mkapa, Prof. Abel Makubi na Makamu Mkuu wa Chuo cha Dodoma Prof. Lughano Kusiluka kwa kuruhusu timu hii kuja  kutujengea uwezo. Huu ni uthibitisho kuwa ushirikiano baina ya hospitali  hizi, unaokoa maisha ya watanzania" Amesema Sr. Dkt. Massenga

 

Daktari Bingwa Mbobezi wa Figo kutoka BMH Sabina Mmbali amesema kuwa Programu hii ya Mashirikiano ya BMH na UDOM kuiwezesha Bugando kuanza kutoa matibabu ya kupandikiza figo imeanza miaka miwili iliyopita ikaenda hatua kwa hatua hadi kufikia mgonjwa wa kwanza kupandikizwa Figo Aprili 16, 2026 na kwa mujibu wa programu hiyo, mashirikiano haya yataendelea hadi hapo Hospitali ya Bugando  itakapofikia hatua ya kutoa matibabu haya yenyewe na kufanya kila kitu.

 

Nae Kiongozi wa Jopo lililompandikiza Figo Mgonjwa huyo wa kwanza Hospitalini hapo Prof. Masumbuko Mwashambwa kutoka UDOM na BMH amesema kuwa Sehemu ya kwanza miaka miwili iliyopita ilikuwa kukagua uwezo wa Hospitali ya Bugando, miundombinu yao, timu ya Wataalamu, madawa na vipimo vinavyohitajika na kutoa maelekezo ya kitaalamu kuhusu maandalizi muhimu.

 

"Baada ya kujiridhisha maandalizi yote yamefanyika, hatua zilizofuatia zilikuwa kufanya maandalizi ya timu za wagonjwa wa kupandikizwa figo na ndugu watakaowqchangia figo hizo; aidha, tuliwafanyia mafunzo muhimu timu ya Bugando baada ya mambo yote kukamilika, tuliingia kwenye hatua ya kupandikiza figo mgonjwa wa kwanza kwa mafanikio Hospitalini hapo" aliongezea Prof. Mwashambwa.

 

Hii ni hatua kubwa katika miaka kumi ya BMH katika kuwajengea uwezo Hospitali nyingine na kuzishusha zaidi huduma zake kwa wananchi katika mikoa mingine.