BMH IMEANZA UZALISHAJI WA DAWA AMBAZO HAZIPATIKANI SOKONI KWA AJILI YA KUKIDHI MAHITAJI YA MTEJA
Na Jeremia Mwakyoma
Picha na Gladys Lukindo
DODOMA - MACHI 11, 2026
Mkurugenzi wa Idara ya Pharmacy ya Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) Amani Msami amesema Pharmacy ya BMH imeanzisha utengenezaji wa dawa ambazo hazipatikani kwenye soko la dawa ambazo zinazingatia mahitaji maalumu ya mgonjwa ili kufanikisha matibabu yake.
Msami amebainisha hilo wakati wa kikao cha mafunzo ya Afya Hospitalini hapo huku akisisitiza ubora wa dawa hizo wanazotengeneza.
"Katika kutengeneza dawa hizi, tunazingatia viwango vya ubora, utunzaji wake ni wa kitaalamu na zimekuwa zikitoa matokeo mazuri kwa watumiaji wake" alisisitiza Msami.
Akiwasilisha mada katika kikao hicho, Mteknolojia dawa wa BMH Petro Alex amesema kwa sasa wanatengeneza dawa za watoto za maji, dawa za Ngozi (Topical Preparations), Vipukusi vya kuua vijidudu visababishi vya magonjwa (Disinfectancts), vipodozi tiba na Maji yenye viambata vya kuzuia wadudu kuota ambayo yanatumika kutengenezea dawa mbalimbali (Preserved Water).
Akitoa ushuhuda baada ya kutumia dawa hizo zinazotengenezwa na Pharmacy ya BMH, Bi. Veronica Gwisu ameelezea kwamba, kwa muda mrefu alikuwa na tatizo la mikono kukauka kuwa mikavu na ngozi ngumu, na alipofika BMH akapata matibabu na kutengenezewa dawa; ndani ya wiki mbili ngozi ya mikono yangu ikarudi kwenye ulaini wake wa asili, dawa haichubui rangi ya Ngozi na haina harufu.
Akitoa maelekezo Mkurugenzi Mtendaji wa BMH Prof. Abel Makubi amebainisha kuwa tayari Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa ametoa maelekezo kuhusu uanzishwaji wa viwanda vya dawa na kuwataka wataalamu wa BMH kuja na wazo la uzalishaji wa dawa.
"Tunawashukuru Wataalamu kwa hiki mlichoanza ni hatua nzuri, lakini ni muhimu sasa kutekeleza maelekezo ya Mhe. Wazari wa Afya kuelekea kwenye viwanda vya uzalishaji dawa, nawaelekeza kuja na wazo pana la uzalishaji wa dawa, wazo hilo lipatikane ndani ya mwezi mmoja" alielekeza Prof. Makubi.