BODI YA WAKURUGENZI YA BMH WASHUKURU HATUA YA MSAJILI WA HAZINA KUTAMBUA MCHANGO WAKE KATIKA UBORA NA HUDUMA ZA MATIBABU NCHINI
Na Jeremia Mwakyoma na Jeremiah Mbwambo
DODOMA - JULAI MOSI, 2026
Kufuatia Msajili wa Hazina Ndg. Nehemia Mchechu kuitaja Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kama Taasisi kinara katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi miongoni mwa Mashirika ya Umma ambayo hayafanyi biashara yanatoa huduma wakati wa hafla ya kumkabidhi Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Gawiwo kutoka mashirika ya Umma, Bodi na Menejiment ya BMH wameshukuru kwa hatua hiyo muhimu.
Akizungumza wakati wa kikao cha mafunzo elekezi kwa wajumbe wa Bodi ya Wadhamini ya BMH, Mwenyekiti wa Bodi Prof. Edward Hosea amesema hatua hiyo ni muhimu kwa kuwa inatambua kuwa utoaji huduma bora kwa wananchi pia unatumia uwekezaji na rasilimali nyingi ikiwemo rasilimali fedha na kutaka Bodi, Menejini na Wafanyakazi wa BMH kwa pamoja kuongeza chachu katika utendaji.
"Hongera kwa Bodi, Menejimenti na Wafanyakazi wote wa BMH kwa hatua hiyo; hii ikawe chachu ya kuboresha zaidi, kujenga uwezo zaidi na kuhakikisha BMH inaendelea kuwa Taasisi inayoongoza katika utoaji huduma bora za Afya hapa nchini na nje ya nchi kwa kuvutia Tiba Utalii.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa BMH Prof. Abel Makubi ameshukuru kazi kubwa iliyofanyika katika miaka 10 ya utoaji huduma ya BMH tangu kuanzishwa kwake ikiwemo kuanzisha huduma za ubingwa 20 na ubobezi 17; na kubainisha kazi kubwa iliyopo mbele kwa sasa kwa Bodi mpya ya BMH, Menejimenti na Watumishi ni kuendeleza mazuri yote yaliyopo na kuanzisha mengine zaidi.
"Tuna kazi kubwa ya kuifanya BMH kuwa Hospitali ya kimataifa , kuwa kinara katika utoaji huduma bora za Afya hapa nchini na hata nje ya nchi kwa kukuza tiba utalii, mashirikiano ya kimataifa na uanzishaji kijiji cha matibabu kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) huku tukizitumia vizuri 4R za Mhe. Rais" alisisitiza Prof. Makubi.
Nae Mwakilishi wa Msajili wa Hazina Bi. Neema Msomba ameahidi kuwa Ofisi ya Msajili wa Hazina itatoa ushirikiano mkubwa na wakati wote milango itakuwa wazi kwa Bodi na Menejimenti ya BMH; itaendelea kusimamia.kwa karibu uwekezaji uliofanywa na Serikali hapo BMH na kusimamia uendeshaji wake.