BMH YAHITIMISHA KAMBI YA UCHUNGUZI WA MAGONJWA NA ELIMU KWA WATUMISHI 98 WA WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM

Published: Nov 12, 2025
BMH YAHITIMISHA KAMBI YA UCHUNGUZI WA MAGONJWA NA ELIMU KWA WATUMISHI 98 WA WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM cover image

Na Jeremia Mwakyoma

MJI WA SERIKALI MTUMBA - DODOMA

NOVEMBA 11, 2025

 

Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) imehitimisha kambi ya uchunguzi wa magonjwa ya VVU/UKIMWI, Homa ya Ini, Afya ya Akili na Magonjwa sugu yasiyo ya kuambukizwa kwa Watumishi wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalumu. 

 

Katika kambi hiyo ya siku mbili, pamoja na uchunguzi wa magonjwa, pia ilihusisha kutoa elimu kwa Watumishi wa Wizara hiyo ya namna ya kujikinga na Magonjwa hayo ambapo takribani Watumishi 98 wa Wizara hiyo wamenufaika na huduma zilizokuwa zinatolewa katika kambi hiyo iliyofanyika katika Mji wa Serikali Mtumba. 

 

Kwa upande wake  Salome Lubasa mratibu wa VVU/UKIMWI na Magonjwa yasiyo ya kuambukizwa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum amesema utekelezaji wa muongozo wa VVU/UKIMWI mahala pa kazi na magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza una manufaa makubwa kwa Watumishi. 

 

"Watumishi wamepata fursa ya kupima magonjwa wakiwa hapahapa ofisini mtumba, wamejua hali zao na wamepewa elimu ya kujikinga na Magonjwa hivyo inasaidia kuwa na Afya njema ya mwili na akili na kuimarisha ufanisi wao wa utendaji kazi" alimalizia Bi. Salome Lubasa.

 

Nae Bi. Azya Mkasha ambaye ni msimamizi wa Mawasiliano ya simu ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalum ameshukuru uongozi wa Wizara kwa kushirikiana na BMH, kuwa Elimu waliyoipata itawasaidia katika kubadili mtindo wa maisha na ulaji wenye Afya, itasaidia Wizara kuwa na Watumishi wenye Afya imara, ni matarajio yake kuwa utendaji wa Watumishi mahala pa kazi utaimarika zaidi.

 

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya ndani wa BMH Happy Kassim amepongeza mwamko wa Watumishi umekuwa mkubwa ametoa wito kwa Wizara na Taasisi nyingine ziendelee na programu za uchunguzi wa Afya kwa watumishi wao mahala pa kazi na utoaji elimu kwa kuzingatia Watumishi wana majukumu mengi na wakati mwingine wanaweza kuwa na ratiba ngumu.