MKURUGENZI MTENDAJI WA BMH PROF. MAKUBI ATAJA MUELEKEO WA BMH UTAKAO IMARISHA UTOAJI WA HUDUMA BORA ZAIDI KWA WANANCHI

Published: Mar 23, 2026
MKURUGENZI MTENDAJI WA BMH PROF. MAKUBI ATAJA MUELEKEO WA BMH UTAKAO IMARISHA UTOAJI WA HUDUMA BORA ZAIDI KWA WANANCHI cover image
  • Huduma bora kwa teknolojia za kisasa,
  • Kuanzisha kituo cha BMH katikati ya Jiji la Dodoma
  • Kuanzisha mfuko wa kusaidia matibabu yenye gharama kubwa (Benjamin Mkapa Hospital Foundation)
  • Kuanzisha Taasisi za Moyo na Macho
  • Kujenga Hostel kwa ajili ya ndugu wa Wagonjwa na Wanafunzi
  •  

Na Jeremiah Mbwambo, Jeremia Mwakyoma
DODOMA - MACHI 12, 2026

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) Prof. Abel Makubi amesema kuwa uelekeo wa BMH ni kuendelea kutoa huduma bora zaidi za Afya kwa Wananchi kwa kutumia teknolojia za kisasa.

 

Ameyasema hayo wakati wa kikao cha Watumishi wote wa BMH kikiangazia tathimini ya utendaji katika kipindi cha miezi 7 iliyopita na muelekeo wa BMH akibainisha pia kuwa suala la uanzishaji wa kituo cha BMH katikati ya Jiji la Dodoma kwa ajili ya kuhudumia wananchi umefikia hatua nzuri.

 

"Tumefanikiwa kupata eneo zuri mjini Dodoma kwa msaada wa viongozi wetu wa Kitaifa, eneo lina nafasi nzuri, majengo yanayofaa kutolea huduma, kamati ya kuandaa na kukamilisha eneo hilo imefikia hatua nzuri na kliniki hiyo ya mjini itatoa huduma za kisasa na fursa kwa Wananchi wengi zaidi kutibiwa kwenye eneo hilo la mjini" alisisitiza Prof. Makubi.

 

Katika hatua nyingine Prof. Makubi amesema BMH iko mbioni kuanzisha mfuko maalumu wa kusaidia wananchi matibabu yenye gharama kubwa ikiwemo upandikizaji Uloto kwa watoto wenye Sickle Cell na Upandikizaji Figo (Benjamin Mkapa Hospital Foundation).

 

"Viongozi na Wadau wengine wameonesha kuunga mkono suala hili na tunatarajia kuzindua mfuko huu wakati wa Kilele cha maadhimisho miaka 10 ya BMH Mei 8, 2026, mfuko utasaidia upatikanaji wa rasilimali muhimu za kusaidia huduma za Afya kwa wananchi" alifafanua Prof Makubi.

 

Prof Makubi aliongeza kuwa BMH inaendelea na mpango wake wa kujenga Taasisi ya moyo na Taasisi ya macho kwa ajili ya kuimarisha matibabu ya magonjwa hayo, mafunzo na tafiti zake; kadhalika inaendelea na mpango wake wa  kujenga Hostel kwa ajili ya wanandugu wanaokuja kuuguza wagonjwa wao na Wanafunzi wa chuo cha Afya cha Benjamin Mkapa.