BMH WAPANUA WIGO WA TIBA UTALII KWA MALAWI

Published: Jan 18, 2026
BMH WAPANUA WIGO WA TIBA UTALII KWA MALAWI cover image

 

Na Ludovick Kazoka, Dodoma-16 January, 2026

 

Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), ambayo ni Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kati kwa Tanzania, imepanua wigo wa tiba utalii kwa nchi ya Malawi hivyo kuwezesha wananchi kutoka nchi hiyo ya kusini mwa Afrika kupata huduma za kibingwa na ubingwa bobezi katika BMH.

 

Waziri wa Afya na Usafi wa Mazingira wa Malawi, Mhe. Madalitso Baloyi, amesema   leo alipotembelea BMH, kuwa wananchi wa Malawi sasa wanaweza kupata matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi nchini Tanzania.

 

 

"Mahusiano katika sekta ya afya yatasaidia wataalamu wetu kubadilishana uzoefu pia wananchi wa Malawi kuja kupata huduma za kibingwa na ubingwa bobezi hapa BMH," amesema Waziri wa Afya na Usafi wa Mazingira wa Malawi alipotembelea BMH leo.

 

 

"Nchini Malawi tuna idadi kubwa ya wagonjwa tunaowapeleka nje ya nchi kwa matibabu, na mara nyingi tunawapeleka nchi ambazo ziko mbali sana, Hali hii huongeza gharama kubwa, hasa gharama za usafiri na matibabu kwa serikali, hivyo basi, tupo hapa BMH kuangalia namna bora ya kushirikiana na jirani yetu Tanzania, na jinsi ya kutumia vyema ukaribu wa kijiografia uliopo katika kupata huduma za kibingwa na kibobezi" alisisitiza Waziri Baloyi.

 

Mhe. Waziri Baloyi ametembelea na kujionea huduma za moyo na kliniki ya wateja mashuhuri na kimataifa  na uchunguzi wa Afya wa kibingwa na ubingwa bobezi.

 

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Prof Abel Makubi, amesema kuwa takribani wageni  400 kutoka nchi mbalimbali zinazotuzunguka  wamepatiwa matibabu katika Hospitali ya Benjamin Mkapa kuanzia  kipindi cha mwaka 2016 hadi sasa.

 

"Ziara hii ya Waziri wa Afya wa Malawi hapa Hospitali ya Benjamin Mkapa inaendeleza mafanikio ya ziara iliyofanywa na Viongozi wa  Hospitali ya Benjamin Mkapa nchini Malawi mwezi Desemba 2025, ambapo tuliweka msingi thabiti wa ushirikiano, tulibaini maeneo muhimu ya ushirikiano, yakiwemo utoaji wa huduma za afya, ujenzi wa uwezo kwa watumishi wa afya, kubadilishana ujuzi, pamoja na kuendeleza utalii wa tiba katika ukanda wetu" alisisitiza Prof. Makubi