BMH KWA KUSHIRIKIANA NA TAASISI YA AFYACHECK WAPELEKA HUDUMA ZA UCHUNGUZI NA MATIBABU KWENYE SOKO LA MACHINGA BAHI ROAD DODOMA

Published: Feb 17, 2026
BMH KWA KUSHIRIKIANA NA TAASISI YA AFYACHECK WAPELEKA HUDUMA ZA UCHUNGUZI NA MATIBABU KWENYE SOKO LA MACHINGA BAHI ROAD DODOMA cover image

 

 

Na Jeremia Mwakyoma

DODOMA - FEB 8, 2026 

 

Kaimu Mkurunzi wa huduma Mkoba kutoka BMH Dkt. Emiliana Myovela amesema kuwa BMH kwa kushirikiana na taasisi ya AfyaCheck wameamua kufanya kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu kwenye soko la Machinga Bahi Road Dodoma ili kuwasogezea huduma karibu  wafanyabiashara kwenye soko hilo na Wananchi kwa ujumla huku akibainisha mwitikio wa kuridhisha wa wananchi. 

 

"Katika Kambi hiyo ya siku tatu tangu Ijumaa, Februari 8, tumeshuhudia mwitikio mkubwa wa wafanyabiashara na Wananchi takribani 1128 ambao walifika kupata huduma jambo linaloonesha uhitaji wao wa huduma za Afya ni Mkubwa " alibainisha Dkt. Myovela huku akitaja orodha ya huduma zilizokuwa zikitolewa kwenye kambi hiyo ni pamoja na magonjwa ya ndani, upimaji wa macho, Ustawi wa Jamii, Uchunguzi wa masikio, koo na pua, Uchunguzi wa afya kwa kina mama na watoto, Uchunguzi wa afya kwa kutumia Ultra Sound, huduma ya afya ya kinywa na meno, na ushauri wa kisaikolojia. 

 

Nae Mkurugenzi wa Taasisi ya AfyaCheck Dkt. Isaac Maro amesema kuwa kambi hiyo ya pamoja kati ya BMH na Taasisi yake ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano ya ushirikiano ambayo Taasisi hizo mbili zilikubaliana na kusaini hati ya makubaliano. 

 

Dkt. Maro aliongeza kuwa mipango iliyopo ni kuendelea kushirikiana na BMH kuandaa kambi hizo zaidi na kupeleka huduma za Ubingwa na Ubingwa Bobezi kwenye maeneo mbalimbali ya nchi na nje ya nchi kwenye nchi zinazotunzunguka kama moja ya njia ya kukuza Tiba Utalii na kuongeza idadi ya Wagonjwa kutoka nchi zinazotuzunguka kuja kutibiwa Tanzania hapo BMH. 

 

Mbunge wa jimbo la Dodoma Mjini Mhe Paschal Chinyele ameshukuru taasisi ya BMH na AfyaCheck kwa kupeleka huduma hizo za Afya kwani moja ya vipaumbele muhimu kwenye jimbo hilo la Dodoma mjini ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya. 

 

"Jambo zuri la kupongeza Taasisi hizi mbili  katika kambi hii ni kuona huduma za Afya zikitolewa bila malipo jambo ambalo limewapa fursa hadi Wananchi wasio na kipato kuweza kupata huduma" alibainisha  Mhe. Chinyele.