BMH KUJA NA KLINIKI JUMUISHI TEMBEZI KWA AJILI YA UPIMAJI BURE WA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA IKIWEMO SARATANI
Na Gladys Lukindo
DODOMA - OKTOBA 8, 2026
Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) imekuja na mpango wa kupeleka kliniki inayotembea katika maeneo mbalimbali ya Dodoma kila mwezi, ikiwamo masoko, ili kuwafikishia wananchi huduma za uchunguzi, vipimo na matibabu bila kulazimika kufika hospitalini.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa BMH Prof. Abel Makubi wakati akizindua kambi ya uchunguzi na matibabu ya kibingwa na ubingwa wa juu huku walengwa wakiwa mama lishe, madereva wa bodaboda na bajaji, mabasi na malori inayofanyika katika Soko la Machinga Complex jijini Dodoma.
Prof. Makubi amesema huduma hizo zitahusisha uchunguzi wa shinikizo la damu, kisukari, magonjwa ya moyo na afya ya akili, na wananchi watapewa elimu kuhusu namna ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza na hatua za kuchukua endapo vipimo vitaonyesha dalili za ugonjwa.

Ameongeza kuwa wananchi watapatiwa huduma za uchunguzi wa saratani, ikiwamo saratani ya shingo ya kizazi na saratani ya matiti, kupitia gari maalum la kliniki inayotembea linalotumika kuwafikishia huduma wananchi katika maeneo yao.
“Huduma hiyo ya uchunguzi wa saratani imewezeshwa kwa ushirikiano na wadau wa afya, akiwamo Taasisi ya Aga Khan pamoja na Serikali ya Ufaransa, kwa lengo la kuongeza wigo wa huduma za uchunguzi na kubaini wagonjwa mapema, “ amesema Prof. Makubi.
Mbali na huduma hizo, wananchi pia wamepatiwa uchunguzi wa ukosefu wa damu (anemia) pamoja na ugonjwa wa seli mundu (sickle cell), huku wale waliobainika kuwa na changamoto wakielekezwa kupata huduma zaidi za matibabu na ushauri wa kitaalamu.
Prof. Makubi ameongeza kuwa kutokufanya uchunguzi wa afya kwa wakati kunaweza kusababisha madhara makubwa, ulemavu na hata vifo, jambo linaloifanya huduma ya uchunguzi wa kinga kuwa muhimu katika kupunguza mzigo wa magonjwa katika jamii.
Wananchi wamehimizwa kufanya uchunguzi wa afya angalau mara moja kwa mwaka na kuufanya kuwa sehemu ya utaratibu wao wa kawaida, badala ya kusubiri hadi watakapohisi maumivu au dalili za ugonjwa ndipo wafike hospitalini.
Mpango huo pia unalenga kuongeza uelewa kwa makundi mbalimbali ya jamii kuhusu umuhimu wa kuishi maisha yenye afya, ikiwamo kuzingatia lishe bora, kufanya mazoezi, kuepuka matumizi ya tumbaku na pombe kupita kiasi pamoja na kufuata ushauri wa wataalamu wa afya.
Naye, Dkt. Missana Yango, Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Mkoa amesema kupitia kambi hii wananchi watanufaika kufanya uchunguzi wa mapema na itawasaidia kufahamu hali zao za kiafya na kuchukua hatua mapema kabla magonjwa hayajasababisha madhara makubwa.
Bi. Joyce Kimario, Mratibu wa Magonjwa yasiyoambukizwa amesema magonjwa yasiyoambukizwa yanaweza kuwa hatari kwa sababu mara nyingi hayana dalili za mapema, hivyo mtu anaweza kuwa na tatizo la kiafya bila kulifahamu hadi ugonjwa unapokuwa umefikia hatua kubwa, amewasihi wananchi kutumia vizuri kambi hiyo ili kupata matibabu.
Kwa upande Bw. Shaban Simba, Mwenyekiti wa Soko la Machinga, ameishukuru BMH kwa kuwasogezea huduma katika eneo lao la kazi ambapo amesema itawapunguzia gharama za kwenda umbali mrefu kutafuta tiba.
Hospitali ya Benjamin Mkapa inaendelea kupeleka huduma karibu na wananchi kupitia kliniki inayotembea na hii itakuwa rahisi zaidi kuwafikia watu katika maeneo yao ya kazi na makazi, hususan makundi yenye shughuli zinazowafanya kukosa muda wa kufika hospitalini na watu wasiokuwa na uwezo.
