BMH IKO MBIONI KUPATA MPANGO MKAKATI MPYA WA MIAKA MITANO
Na Jeremia Mwakyoma
Picha Gladis Lukindo na Ludovick Kazoka
Morogoro - Novemba 15, 2025
Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) iko mbioni kupata Mpango Mkakati mpya wa miaka mitano (2026 - 2031), Mkurugenzi Mtendaji wa BMH Prof Abel Makubi ameahidi maoni ya Baraza la Wafanyakazi wa BMH kuzingatiwa katika Mpango Mkakati huo.
Hayo yamebainishwa na Prof. Makubi wakati akihitimisha Kikao cha 12 cha Baraza la Wafanyakazi la BMH kilichofanyika katika Hotel ya Cate iliyopo Morogoro.
"Tunaandaa mpango Mkakati mpya wa miaka mitano, katika maandalizi ya mpango huo Baraza la Wafanyakazi la Hospitali litashirikishwa kwa karibu na maoni yenu yatazingatiwa" alibainisha Prof. Makubi.
Prof. Makubi aliongeza kuwa katika uandaaji wa Mpango Mkakati huo, BMH inashirikiana na Wizara ya Afya na pia alielekeza timu ya maandalizi kuhakikisha inashirikisha Watumishi wote wa BMH ili kupata maoni yao kwa upana zaidi.
"Katika kupanua wigo wa ushirikishwaji Watumishi wa BMH, Kamati inayoandaa mpango huu iandae kikao cha Watumizhi wote ili kupata maoni yao" aliongeza Prof. Makubi.
Aliongeza kuwa Mpango huu utaipa BMH muelekeo wa miaka mitano ijayo kwa kuzingatia mpango Mkakati uliopo sasa umeisha muda wake.
Prof. Makubi alilitaka Baraza na Wafanyakazi wote wa BMH kutambua "Sustainability" ya BMH itategemea ubora wa huduma za Afya zinazotolewa kwa Wananchi na Masuala ya kuimarisha uwezo wa kifedha wa Taasisi ili kuweza kugharamia madawa na vifaa tiba kuhudumia Wananchi.
Nae Mteknolojia Moyo Godfrey Tamba ameshauri kuwa programu ya Huduma Mkoba (Outreach Program) itumike kuzifikia Hospitali za Mikoa na Wilaya mbalimbali kuwaelimisha huduma zinazopatikana BMH na kuwafikia Wananchi kwa uchunguzi na elimu zaidi ya magonjwa na huduma.
Mkurugenzi wa Tiba wa BMH Dkt. Kesy Shija akitoa taarifa ya hali ya Utoaji huduma kwa kipindi cha miezi 3 tangu Julai 2025 hadi Oktoba 2025, amesema kuwa idadi ya Wagonjwa wapya waliohudumiwa ni 13,531 na Wagonjwa wa marudio ni 79,115; Wagonjwa waliolazwa walikuwa 4,790; vipimo vya Maabara vilivyotolewa 175,758, jumla ya Vipimo vya Radiolojia 33,743 mtiririko wa Huduma za dawa kwa kipindi cha miezi hiyo mitatu 92,174, Huduma za Upasuaji 866 na Procedure 3513.