BMH YAANZISHA KLINIKI MAALUM YA UPUNGUFU WA DAMU NA KLINIKI JUMUISHI YA MAMA MJAMZITO NA MAGONJWA YA MOYO
Na. Gladys Lukindo na Jeremia Mwakyoma, Dodoma
HOSPITALI ya Benjamin Mkapa (BMH) imeanzisha kliniki maalumu ya kuwahudumia wagonjwa wenye upungufu wa damu na kliniki Jumuishi ya mama mjamzito na magonjwa ya moyo, hususan kwa wanawake wajawazito na watoto, ikiwa ni sehemu ya kuboresha huduma za afya na kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika vinavyotokana na matatizo hayo.
Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Prof. Abel Makubi amesema hayo wakati akizindua kliniki ya upungufu wa damu na kliniki Jumuishi ya mama mjamzito na magonjwa ya moyo ambapo amesema uamuzi wa kuanzisha kliniki hizo umetokana na ukubwa wa tatizo la upungufu wa damu nchini, hasa kwa wanawake wajawazito na Watoto na kupunguza vifo vinzvyotokana na magonjwa ya damu kwa wamama wajawazito.
‘’Takwimu zinaonyesha kuwa kati ya wanawake wajawazito 10, takribani sita wana upungufu wa damu, huku kwa watoto hali hiyo ikiwakumba takribani watano kati ya 10, jambo linalohitaji juhudi za pamoja katika uchunguzi, tiba na utoaji wa elimu kwa jamii, amesema Prof. Makubi.
Prof. Makubi ameongeza kuwa BMH ina wataalamu waliobobea katika magonjwa ya damu, vifaa vya uchunguzi na dawa zinazohitajika, hivyo kliniki hizo zitatoa fursa kwa wagonjwa kupata huduma maalumu na ushauri wa kitaalamu ili kupunguza madhara yanayotokana na tatizo hilo.
.webp)
Nae Mkurugenzi wa tiba BMH Dkt. Jesse Jonathan amemshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa BMH kwa maono na usimamizi uliowezesha kuanzishwa kwa Clinic hizi mbili huku akitoa wito kwa idara nyingine hapo BMH kuhakikisha wagonjwa wote watakaobainika kuwa na dalili za upungufu wa damu au magonjwa ya moyo kwa wajawazito kupatiwa huduma kwenye Clinic hizo na wananchi kujenga utamaduni wa kufanya uchunguzi na matibabu.
Daktari Bingwa wa magonjwa ya damu, Dkt. Irene Mteta, amesema lengo la kliniki hiyo ni kutambua wagonjwa wenye upungufu wa damu, kubaini chanzo cha tatizo na kuhakikisha wanapata matibabu yanayofaa. Amesisitiza kuwa si sahihi kwa mtu kutumia dawa bila kufanyiwa uchunguzi wa kutosha ili kujua kinachosababisha upungufu huo.
Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo, Dkt. John Meda amesema kliniki hiyo itasaidia kuboresha ufuatiliaji wa wanawake kabla ya kupata ujauzito, wanapokuwa wajawazito na baada ya kujifungua, ili kubaini changamoto za kiafya mapema na kuhakikisha mama na mtoto wanapata huduma zinazohitajika katika kipindi chote hicho.
Naye Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Uzazi na Wanawake, Dkt. Zakaria Kombo amesema kliniki ya mama mjamzito na magonjwa ya moyo itajikita katika kubaini na kudhibiti matatizo ya moyo kwa wanawake wajawazito, kwani magonjwa hayo yanaweza kuongeza hatari na madhara makubwa wakati wa ujauzito na kujifungua. Amesema uchunguzi wa mapema na ufuatiliaji wa karibu ni muhimu katika kupunguza hatari hizo.
Kwa upande wake, Beatrice Faustine, mkazi wa Mnada Mpya, ameishukuru BMH kwa huduma alizopata baada ya kufika hospitalini hapo akiwa na tatizo la upungufu wa damu. Amesema huduma hizo zimemsaidia kupata msaada wa kitabibu na kuongeza umuhimu wa wananchi kujitokeza kupima afya zao wanapohisi kuwa na tatizo.