BMH KUELEKEA KUWA HOSPITALI YA TAIFA, MSISITIZO WA UBORA WA HUDUMA UENDELEE KUWA KIPAUMBELE
Na Jeremia Mwakyoma
Picha na Gladys Lukindo
AGOSTI 15, 2026
Menejimenti na Watumishi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) wametakiwa kuendelea kuboresha zaidi ubora wa huduma za Afya zinazotolewa Hospitalini hapo wakati ambapo BMH inaelekea kuwa Hospitali ya Taifa.
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa BMH Prof. Abel Makubi wakati wa kikao cha 14 cha Baraza la Wafanyakazi la BMH kilichofanyika leo jijini Arusha.
"Mchakato wa BMH kuwa Hospitali ya Taifa unaendelea, tukiwa tunasubiri hatua za ngazi husika, jukumu letu kama BMH ni kuendelea kuboresha huduma kama agenda yetu namba moja ya sekta ya Afya na BMH inavyosisitiza kwenye huduma bora za matibabu, mafunzo na utafiti" alisisitiza Prof. Makubi.
Aidha, Prof. Makubi aliwataka Menejimenti na Watumishi wa BMH kuhakikisha wanajikita katika kutekeleza maelekezo ya Wizara yaliyotolewa na Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa (Mb.) akisisitiza uwekezaji wa viwanda vya madawa na vifaa tiba, huduma bora, Bima ya Afya kwa wote, kupata ithibati za kimataifa, kuwekeza katika njia za Kidigitali katika kutoa huduma za Afya na nidhamu kwa watoa huduma mambo ambayo yataongeza idadi ya Wananchi watakaokwenda kutibiwa BMH.
Wakiwasilisha taarifa za utendaji wa BMH kwa mwaka wa fedha 2025/2026 Mkurugenzi wa Tiba na Mkurugenzi wa Mipango na Fedha wamepongeza viwango vilivyofikiwa katika utekelezaji wa malengo yaliyowekwa.
"Katika kipindi cha mwaka 2025/2026, BMH imeona wagonjwa 294,085 ikilinganishwa na wagonjwa 271,109 walioonwa mwaka 2024/2025 sawa na ongezeko la asilimia 8.5, ongezeko hili limetokana na Hospitali kuongeza mikakati ya kuanzisha Royal Clinic, Huduma Mkoba, Kambi za matibabu na Clinic kuanza mapema muda wa kutoa huduma na kuboresha huduma kwa wateja" alifafanua Mkurugenzi wa Mipango na Fedha wa BMH Ambele Msika.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa huduma za Tiba BMH Dkt. Jesse Kashabano amesema kuwa huduma za tiba zimeboreka kwa kiwango kikubwa BMH kwa mwaka wa fedha 2025/2026 ikilinganishwa na kipindi kama hiki mwaka wa fedha 2024/2025 na kuwa wagonjwa wameonesha kuridhika kwa kiwango kikubwa na huduma, hivyo kupelekea ongezo la wagonjwa hospitalini kutoka ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake Katibu wa TUGHE Mkoa wa Dodoma Ndugu Samwel Nungwa amepongeza utaratibu wa BMH kutoa kipaumbele kwa Baraza la Wafanyakazi na kutoa wito kwa Menejimenti kuongeza wigo wa ushirikishwaji wa watumishi na wadau katika kutafuta majawabu ya masuala yanayoibuliwa na Watumishi na Wateja wa BMH.