BMH YASHIRIKI KUTOA MAFUNZO NA HUDUMA ZA UCHUNGUZI WA MAGONJWA KWA WATUMISHI WA WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA NA MAKUNDI MAALUMU

Published: Nov 10, 2025
BMH YASHIRIKI KUTOA MAFUNZO NA HUDUMA ZA UCHUNGUZI WA MAGONJWA KWA WATUMISHI WA WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA NA MAKUNDI MAALUMU cover image

Na Jeremia Mwakyoma 

MTUMBA MJI WA SERIKALI - DODOMA

NOVEMBA 10, 2025 

 

Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) imeshiriki kutoa mafunzo na uchunguzi wa magonjwa ya VVU/UKIMWI, homa ya Ini, Afya ya Akili na magonjwa sugu yasiyoambukizwa kwa Watumishi wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalum. 

 

Akifungua programu hiyo ya mafunzo na uchunguzi wa Afya kwa Watumishi, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Wakili Amon Mpanju amesema kuwa programu hiyo ni utekelezaji wa Mwongozo wa kudhibiti magonjwa hayo mahala pa kazi na ameishukuru BMH na Wataalamu wake kwa kuungana na Wizara katika utekelezaji. 

 

"Nimeambiwa kuwa idadi ya Watumishi waliojitokeza kufanya uchunguzi wa magonjwa imekuwa kubwa, na hiki ni kiashiria kizuri, kusimamia Afya za Watumishi kutahakikisha Watumishi kuwa na Afya bora jambo linaoongeza ufanisi wa kazi; na elimu mliyoipata Watumishi  mkaipeleke kwenye familia zenu" alisisitiza Naibu Katibu Mkuu Mpanju. 

 

Aliwasisitiza watumishi  kwa kushirikiana na Uongozi kuweka utaratibu wa kufanya mazoezi na kuimarisha klabu ya mazoezi ya watumishi wa Wizara kwa kuzingatia kuwa michezo inafaida kubwa katika kuimarisha na kulinda Afya. 

 

Nae Daktari Bingwa Mbobezi wa Magonjwa ya Akili na Uraibu wa BMH Isack Rugemalila amebainisha kuwa karibu asilimia 15 ya Watumishi kwenye maeneo ya kazi wana changamoto za Magonjwa ya Akili au wanaishi na viashiria vya Afya ya Akili na baadhi ya visababishi ni pamoja na matumizi ya pombe na dawa za kulevya. 

 

Dkt. Rugemalila ameongeza kuwa changamoto hiyo inaathiri Utendaji kazi wa Watumishi na taasisi kwa ujumla na kupunguza matokeo tarajiwa ya kazi na utoaji Huduma. 

 

Nae Daktari wa Magonjwa ya Ndani wa BMH Happy Kassim akizungumzia Magonjwa yasiyo ya kuambukiza amesema kuwa karibu asilimia 41 ya vifo hapa nchini vinasababishwa na magonjwa yasiyo ya kuambukizwa hivyo kuchukua hatua za makusudi za kupambana na visababishi vya magonjwa hayo ni muhimu sana kama ulaji wa vyakula bora vyenye kujenga na kulinda Afya na kubadili mfumo wa maisha hasa kuachana na tabia bwete na kusisitiza umuhimu wa Watumishi kufanya uchunguzi/kupima Afya zao.