BMH YAAHIDI KUAANDAA MAFUNZO YA KUJENGA UWEZO NA HUDUMA KWA MTEJA KWA AJILI YA HOSPITALI NA VITUO VYA AFYA KUTOKA MIKOA YA JIRANI

Published: Aug 27, 2026
BMH YAAHIDI KUAANDAA MAFUNZO YA KUJENGA UWEZO NA HUDUMA KWA MTEJA KWA AJILI YA HOSPITALI NA VITUO VYA AFYA KUTOKA MIKOA YA JIRANI cover image

Na Jeremia Mwakyoma

PICHA GLADYS LUKINDO - AGOSTI 27, 2026

Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) imepokea ugeni wa viongozi na wataalamu kutoka Hospitali za Rufaa za Mikoa ya Dodoma na Manyara waliofika BMH kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu katika masuala ya utoaji huduma bora za Afya kwa Wananchi.

 

Katika ziara hiyo, BMH imeahidi itaandaa mafunzo ya kujenga uwezo zaidi na kuboresha huduma kwa mteja maalumu kwa ajili ya Hospitali na Vituo vya Afya kutoka mikoa ya jirani na Dodoma, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa BMH Dkt. Abdallah Baja amesema lengo ni kuhakikisha Hospitali zetu zinatoa huduma kwa wananchi zenye kiwango cha ubora wa hali ya juu.

 

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha udhibiti Ubora BMH Dkt. Paul Kuzungu amesema mafunzo hayo yataandaliwa na kutolewa kupitia maabara maalum za mafunzo za BMH (Skills Lab).

 

Washiriki wa ziara hiyo wamepongeza  BMH kuwa ni Hospitali ambayo imepangwa vizuri ikapangika, ina mazingira mazuri ya utoaji huduma kwa wananchi na watumishi wake wamejipanga vizuri kuwahudumia wananchi.

 

"Tumejifunza kuwa mazingira mazuri ya kazi, usafi wa hali ya juu wa Hospitali vinachangia watumishi kila mmoja kwenye eneo lake kuwa na ari ya kazi na kuweza kutoa huduma bora kwa mteja"  alisisitiza Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma Dkt. Baraka Mponda.

 

Dkt. Mponda aliongeza kuwa ujumbe wao umeshuhudia BMH ilivyoweka mifumo mizuri ya kutoa taarifa kwa wateja wake na kupokea malalamiko na hoja mbalimbali zinazotoka kwa wateja kwa kutumia njia za kidigitali zinazoweza kukutanisha wateja na uongozi wa hospitali jambo linalosaidia kuwaweka wananchi karibu na uongozi wa Hospitali.

 

Hospitali hizo za Rufaa za Mikoa ya Manyara na Dodoma  wameahidi kukuza na kuboresha zaidi mashirikiano na BMH ili kuwarahisishia wagonjwa ambao wanatoka mikoa hiyo kwa rufaa kuja kutibiwa BMH.