BMH YATOA ELIMU YA MAGONJWA YASIYO YA KUAMBUKIZA NA KUFANYA UPIMAJI AFYA KWA WATUMISHI WA NMB DODOMA.
Na Jeremia Mwakyoma
DODOMA - SEPTEMBA 10, 2025
Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) leo imeendesha programu ya utoaji elimu ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwa Watumishi wa bank ya NMB Dodoma na kuwafanyia uchunguzi wa vipimo vya Afya kubaini magonjwa hayo yasiyo ya kuambukiza.
Uchunguzi ulihusisha magonjwa ya moyo, macho na mifupa kwa kufanywa na timu ya Madaktari Bingwa Wabobezi na Wataalamu wengine wa Afya kutoka BMH.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya moyo wa BMH Digna Riwa amebainisha kuwa kumekuwa na ongezeko la magonjwa yasiyo ya kuambukiza (NCDs) hivyo BMH imeamua kuweka programu ya kutoa elimu kwa Watumishi wa Taasisi mbalimbali na kufanya vipimo vya Afya.
Daktari Bingwa wa Mifupa na Ajali Dkt. Saguda Nilla wakati wa kutoa elimu amesema magonjwa yasiyo ya kuambukiza yanaweza kuathiri hali za Afya za Watumishi na kuathiri utendaji wao hivyo ametoa wito kwao kuanzisha utamaduni wa kufanya uchunguzi wa Afya zao wa kina pasipo kusubiri hadi waanze kuugua.
"BMH tumeanzisha huduma za uchunguzi wa Afya wa Kina (master health check up) zinazotolewa kwenye Kliniki ya Wateja Maalum, Wateja wa Kimataifa na Uchunguzi wa Afya wa Kina ambapo ni fursa kwa watumishi wa Taasisi na Wananchi kufanya uchunguzi wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza" amebainisha Dkt. Saguda.
Akiongea wakati wa kufunga Mafunzo hayo kwa watumishi wa NMB, Kaimu Meneja wa Kanda Ndg. Amos Mubusi ameshukuru ushirikiano uliopo kati ya NMB na BMH.
"Mahusiano haya yataongeza wepesi wa wafanyakazi wa NMB kupata huduma za uhakika za afya na kwa haraka zaidi pale BMH kupitia Kliniki ya Royal" alisisitiza Ndg. Mubusi.
Meneja wa Huduma Sambazishi wa NMB Kanda ya Kati Ndg. Nkuba Mashita ameshukuru kwa fursa ya uchunguzi wa afya kwa Watumishi na kusema itawawezesha kuchukua hatua za mapema endapo itaonekana kuna uhitaji ukizingatia Mtindo wa maisha kwa watu wengi kwa sasa na aina ya kazi wanazofanya unachangia magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Meneja Mahusiano Kitengo cha Wateja Maalum Binafsi wa NMB Pendo Ngoi amesema hali ya sasa vijana watoto unakuta wanaugua magonjwa yasiyoambukiza, hivyo ametoa wito wa kubadili mtindo wa maisha, ulaji usio wa Afya na kufanya mazoezi ya mwili.