BMH YATOA HUDUMA ZA MATIBABU YA KIBOBEZI KWENYE MAONESHO YA TISA YA KITAIFA YA TEKNOLOJIA ZA MADINI MKOANI GEITA

Published: Sep 29, 2026
BMH YATOA HUDUMA ZA MATIBABU YA KIBOBEZI KWENYE MAONESHO YA TISA YA KITAIFA YA TEKNOLOJIA ZA MADINI MKOANI GEITA cover image
Na Jeremia Mwakyoma
GEITA - SEPT 27, 2026
 
 
Katika Maonesho hayo, Daktari Bingwa wa magonjwa ya Damu kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) ametoa wito kwa wadau wa sekta ya madini wanaoshiriki maonesho hayo na wananchi wa Geita kwa ujumla  kutembelea banda la BMH ili kufanya vipimo vya ugonjwa wa Selimundu (Sicle Cell) na kujua kama wana vinasaba vinavyoweza kusababisha kuzaa mtoto mwenye ugonjwa wa Selimundu.
 
 
"BMH tumekuwa tukipokea wagonjwa wengi wenye ugonjwa wa Selimundu kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa, Geita na Shinyanga, wakati mwingine hawajui hali zao na unaweza kukuta  wazazi wamepata mtoto mwenye ugonjwa huo  bila kuwa na uelewa matokeo yake wanachelewa kumuwahisha Hospitali kwenye  matibabu ya uhakika hivyo kusababisha madhara zaidi" alielezea Dkt. Mhando.
 
Aliongeza kuwa katika maonesho haya BMH imeleta huduma za uchunguzi na vipimo vya ugonjwa huo, elimu na ushauri wa kitaalamu na kutoa wito kwa wadau wa Maonesho hayo ya madini kutembelea banda la BMH kufanya vipimo. Dkt. Mhando pia amebainisha kuwa BMH inatoa vipimo na ushauri kwa wale wanaotarajia kuwa wana ndoa ili kujua kama wako salama kuzaa au kuna uwezekano wa kuzaa mtoto mwenye ugonjwa wa Selimundu.
 
 
 
 
Nae Daktari Bingwa Bobezi wa Magonjwa ya Ndani wa BMH Dkt. Sophia Muhali amewaalika Wadau wa madini kutembelea Banda la BMH kupata vipimo, elimu na ushauri  wa magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) kama shinikizo la damu, sukari na pia magonjwa mengine ya kuambukiza ikiwemo homa ya inni.
 
 
Kwa upande wake Mteknolojia Dawa wa BMH Petro Alex pamoja na kutoa huduma ya dawa kwa waliotembela banda la BMH ameendelea kutoa elimu ya matumizi sahihi ya dawa ili  kupunguza tatizo la Usugu wa Vimelea dhidi ya dawa (UVIDA).