BMH YAPOKEA MADAKTARI BINGWA WABOBEZI KUTOKA CHINA, WATAKUWA BMH WAKITOA HUDUMA KWA MIAKA MIWILI
Na Ludovick Kazoka na Gladys Lukindo, Dodoma Aprili 17, 2026
Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) imepokea timu ya Madaktari Bingwa Wabobezi watano kutoka China, watakaohudumu katika Hospitali hii ya Rufaa ya Kanda kwa muda wa miaka miwili.
Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Prof Abel Makubi, ameishukuru Serikali kwa kuleta madaktari hao.
"Tunaishukuru Serikali kwa kuleta madaktari bingwa hawa kutoka China. Wataalamu hawa watatusaidia kupanua wigo wa huduma zetu hapa BMH, Timu iliyokuja inajumuisha Madaktari Bingwa Wabobezi wa Tiba Asili za Kichina, Upasuaji wa Ubongo, Mishipa ya Fahamu na Uti wa Mgongo, Upasuaji wa Mikono na Miguu, Upasuaji Mifupa na magonjwa ya Moyo " amesema Prof Makubi.
Prof Makubi amefafanua kuwa wataalamu hao watasambazwa katika idara mbalimbali za BMH.
"Taasisi itawapatia ushirikiano mkubwa muda wote wa kuhudumia BMH," ameongeza Prof Makubi.
Kwa upande wake, Kiongozi wa msafara kutoka timu ya madaktari kutoka China, Dkt. Liu Jia, anasema amefurahishwa kufanya kazi na BMH kwa mara ya kwanza.
"Programu hii ni matokeo ya uhusiano mzuri wa kidiplomasia wa muda mrefu kati ya Tanzania na China," amesema Dkt Jia.
Aidha mwakilishi kutoka Wizara ya Afya, Ndg. Marcelo Kaijage, anasema Serikali ya Tanzania imekuwa na ushirikiano wa muda mrefu na Serikali ya China katika sekta ya afya.
" Hii ni fursa kwa watanzania, naomba wajitokeze kupata huduma kwa wataalamu hawa wanaoenda kushirikiana na wataalamu wetu," amesema Ndg. Kaijage.