HUDUMA ZA FIGO NA ULOTO ZINAZOTOLEWA BMH ZATAJWA KUIFANYA TANZANIA KUWA KITOVU CHA TIBA UTALII

Published: Jul 20, 2026
HUDUMA ZA FIGO NA ULOTO ZINAZOTOLEWA BMH ZATAJWA KUIFANYA TANZANIA KUWA KITOVU CHA TIBA UTALII cover image

Na. Jeremiah Mbwambo, Jeremia Mwakyoma

Picha: Gladys Lukindo
DODOMA - JULAI 16, 2026

WAZIRI wa Afya, Mohamed Mchengerwa (Mb.) amesema uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika sekta ya afya hususani Hospitali ya Benjamin Mkapa umeifanya Tanzania kuacha kusafirisha wagonjwa wengi nje ya nchi kwa matibabu ya figo na uloto, badala yake kuanza kupokea wagonjwa kutoka mataifa mengine kufuata huduma hizo.

Mchengerwa aliyasema hayo katika hafla ya uchangishaji fedha kwa ajili ya Mfuko wa Upandikizaji wa Figo na Uloto iliyoandaliwa kwa ushirikiano wa BMH na UWT.

"Hafla hii haikuandaliwa kwa ajili ya chakula, bali kuokoa maisha ya Watanzania wanaohitaji huduma hizo, leo itakumbukwa kwa kuokoa maisha ya watanzania" Amesema Waziri wa Afya

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), Prof. Abel Makubi, alimshukuru Waziri Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa, Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) pamoja na wadau wengine kwa kuendelea kuunga mkono kampeni ya uchangishaji fedha kwa ajili ya mfuko huo.

"BMH kwa sasa ina huduma 20 za kibingwa na Kibingwa Bobezi 17, huku hospitali ikiwa imefanikiwa kupandikiza uloto kwa watoto 38 kati yao, mtoto mmoja akitokea nchini Congo DRC na pia kupandikiza Figo watu 56, mafanikio hayo yameleta matumaini mapya kwa familia nyingi nchini" amesema Prof. Makubi

Prof. Makubi alisema kwa sasa watoto 50 na watu wazima 50 bado wanasubiri kufanyiwa upandikizaji wa figo na uloto, huku matarajio yakiwa wadau kuchangia zaidi ya Sh bilioni saba ndani ya miaka miwili kusaidia huduma hizo.

Alisema ndani ya miaka 10 ijayo BMH imejipanga kupanua huduma zake kupitia miradi mikubwa ikiwemo ujenzi wa kituo cha kisasa cha saratani chenye thamani ya Sh bilioni 32 na kituo kikubwa cha huduma za figo, huku pia ikishirikiana na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kuifanya Dodoma kuwa kitovu cha tiba utalii.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, aliipongeza Wizara ya Afya na BMH kwa mafanikio makubwa yaliyofikiwa katika utoaji wa huduma za kibingwa za figo na uloto.

Senyamule alisema mafanikio hayo yanaonyesha namna uwekezaji wa serikali ulivyobadilisha sekta ya afya nchini na kwamba ushirikiano wa wadau umeendelea kuwa chachu ya kuimarisha huduma hizo.

 

Ametoa wito kwa taasisi, makampuni na wananchi kuendelea kuunga mkono kuchangia Mfuko wa Upandikizaji wa Figo na Uloto ili wagonjwa wengi zaidi waweze kupata huduma za matibabu kwa wakati na kuokoa maisha yao.