MADAKTARI BINGWA WA BMH WAHITIMISHA KAMBI YA UCHUNGUZI NA MATIBABU YA MAGONJWA YA NGOZI WILAYANI KONDOA, SASA NI ZAMU YA WILAYA YA BAHI

Published: Jul 04, 2026
MADAKTARI BINGWA WA BMH WAHITIMISHA KAMBI YA UCHUNGUZI NA MATIBABU YA MAGONJWA YA NGOZI WILAYANI KONDOA, SASA NI ZAMU YA WILAYA YA BAHI cover image

Na Jeremia Mwakyoma
BAHI - JUNI 26, 2026

Madaktari Bingwa wa Magonjwa ya ngozi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) leo wameendelea na kutoa huduma ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya ngozi kwa wananchi wa Wilaya ya Bahi kwenye kambi maalumu inayofanyika kwenye Hospitali ya Wilaya ya Bahi.

Mratibu wa Kambi hiyo kutoka BMH Mfamasia Agness Kessy anasema kambi hiyo ilianza katikati ya wiki Wilayani Kondoa ambapo mwitikio wa wananchi ulikuwa wa kuridhisha na baada ya ratiba ya Kondoa kukamilika, leo Madaktari wa BMH wamehamia WilayaniΒ  Bahi wakiendelea kutoa matibabu kwa wananchi wa Bahi.

"Wilayani Kondoa zaidi ya Wagonjwa 100 wamepata huduma za uchunguzi wa magonjwa ya ngozi na matibabu zikiwemo dawa za kutibu magonjwa ya ngozi zinazotengenezwa na Wataalamu wa Dawa wa BMH ambazo zina ufanisi mkubwa wa kutibu magonjwa ya ngozi huku zikiwa zimeondolewa viambata vinavyoweza kusababisha madhara kwenye mwili wa Binadamu" amesisitiza Mfamasia Kessy

Mfamasia Kessy amewaasa wananchi wa Bahi na viunga vyake vyote kutumia fursa hiyo vizuri kwa kujitokeza kwenye kambi hiyo kufanya uchunguzi ili kuweza kubaini mapema changamoto za magonjwa ya ngozi na kupata matibabu sahihi kabla magonjwa hayo hayajawaletea madhara makubwa.


Kwa upande wake Mteknolojia Dawa wa BMH Petro Alex amesema kuwa katika kambi hiyo, wamepeleka Hospitalini hapo Bahi, mashine ya kuchanganyia dawa za ngozi inasaidia kutengeneza dawa kwa urahisi na kutengeneza dawa zenye mchanganyiko sawa wa viambata kulingana na mahitaji aliyoyaainisha Daktari baada ya kumfanyia mgonjwa uchunguzi wa kina.

Nae Daktari wa Magonjwa ya ngozi wa BMH Kahabi Kimotoli amesema katika kambi hiyo wamekuwa wakitibu changamoto za ngozi kuathiriwa na jua, pumu ya ngozi, fangasi, magonjwa ya nywele, magonjwa ya kucha, magaga, chunusi, miwasho sehemu za siri na kuota vinyama/sunzua sehemu za siri (warts), mabaka meupe kwenye ngozi, kutoa harufu vidole vya miguuni na vidonda.Β 

Β