BMH KUANZISHA MFUKO MAALUM WA KUSHIRIKISHA WADAU KUWEZESHA MATIBABU YA UPANDIKIZAJI ULOTO KWA WATOTO WENYE SICKLE CELL NA UPANDIKIZAJI FIGO

Published: Feb 17, 2026
BMH KUANZISHA MFUKO MAALUM WA KUSHIRIKISHA WADAU KUWEZESHA MATIBABU YA UPANDIKIZAJI ULOTO KWA WATOTO WENYE SICKLE CELL NA UPANDIKIZAJI FIGO cover image

Na Jeremia Mwakyoma

PICHA: GLADYS LUKINDO & LUDOVICK KAZOKA

DODOMA - FEB 10, 2026 

 

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) Prof. Abel Makubi wakati wa ziara ya Mheshimwa Mama Anna Mkapa , Mke wa Rais Mstaafu wa Tanzania wa awamu ya tatu alipotembelea BMH kujionea utoaji huduma na mafanikio yaliyopatikana ndani ya kipindi cha miaka 10 ya utoaji huduma. 

 

"Matarajio ya BMH ni kuanzisha rasmi na kuuzindua  mfuko shirikishi wa wadau kuunga mkono juhudi za serikali katika kusaidia Wananchi wenye uhitaji wa kupandikizwa Uloto au Figo  wakati wa sherehe za kilele cha maadhimisho ya miaka 10 tangu Kuanzishwa kwa BMH" alisisitiza Prof. Makubi huku akiongezea kuwa mfuko huo utawezesha wadau mbalimbali kuweza kuunga Mkono juhudi za Serikali kwa kuchangia fedha zitakazosaidia matibabu hayo ambayo yana wastani wa gharama ya milllion 75 kupandikiza Uloto au million 40 kupandikiza figo, kwa kila mgonjwa mmoja. 

 

Prof. Makubi aliongeza kuwa kwa sasa BMH ndio Hospitali pekee hapa nchini na Afrika Mashariki inayotoa huduma za matibabu ya upandikizaji Uloto kwa watoto wenye Sickle Cell na kusaidia kupunguza Rufaa za Wagonjwa kwenda nje ya nchi ambako gharama ni kubwa zaidi  katika kutibiwa ugonjwa huo .Prof Makubi ameeleza juhudi za serikali katika uwekezaji mkubwa ndani ya sekta ya afya zimeokoa fedha nyingi katika eneo hili na sasa umefika muda wa wadau kuunga mkono mafanikio haya makubwa. 

 

Kwa upande wake Mheshimiwa Mama Anna Mkapa amesema ni jambo la faraja kwa Hospitali hii kupewa jina la mume Wake Hayati Mhe. Benjamin Wiliam Mkapa na kuona namna ilivyopiga hatua  kubwa ndani ya kipindi cha miaka 10 ikiwemo kuweza kutoa huduma takribani 20 za ubingwa na 17 za ubingwa wa juu. 

 

Mama Anna Mkapa pia amepongeza dhamira ya Mhe Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwekeza katika Sekta ya Afya na kuwezesha Wananchi kuweza kupata huduma nyingi za ubingwa wa juu na kupunguza rufaa za kwenda nje ya nchi.  Aidha , Mheshimiwa Mama Anna Mkapa ameahidi kusaidia baadhi ya maeneo ya upanuzi wa huduma za upandikizaji figo ili kuendeleza maono ya Hayati Mheshimiwa Rais Mstaafu Benjamin Mkapa ambaye alichangia kwa kiasi kikubwa katika kuanzishwa kwa huduma za matibabu ya figo katika taasisi za BMH/UDOM.