Mwanzo / Huduma Zetu / BMH YATIBU WATOTO 21 WENYE UGONJWA WA SELIMUNDU.

BMH YATIBU WATOTO 21 WENYE UGONJWA WA SELIMUNDU.

Published on June 20, 2025

Article cover image

Na; Carine Senguji na Gladys Lukindo. Juni 19 2025. Dodoma

Ikiwa dunia inaadhimisha siku ya selimundu Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) imefanikiwa kutibu watoto 21 wenye ugonjwa wa selimundu nchini.

Akiongea katika maadhimisho ya siku ya selimundu duniani Mkurugenzi Mtendaji wa BMH amesema kuwa serikali imewekeza 1.7b kwa ajili ya kutokomeza ugonjwa wa selimundu na mpaka sasa watoto 21 wameshapona kabisa.

"Tunamshukuru Rais na serikali kwa ujumla kwa uwekezaji mkubwa wa 1.7b kwa ajili ya matibabu ya watoto wenye ugonjwa wa selimundu na tukiwa tunaadhimisha siku hii ya selimundu duniani tunafuraha kusema kuwa mpaka sasa tumetibu watoto 21 na wamepona kabisa na bado tunaendelea kutoa matibabu kwa watoto wengine lengo ni kutokomeza kabisa ugonjwa huu," amesema Prof. Makubi.

Akiendelea kuzungumza Prof. Makubi amesema BMH inaendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu ugonjwa huu, "Sisi kama BMH tunahakikisha katika kutoa elimu ya uelewa kwa wananchi na kuondoa dhana potofu ambazo zipo katika jamii katika vijiji na miji mbalimbali kwa kufanya huduma mkoba," ameongeza Prof. Makubi.

Prof. Makubi ameendelea kwa kuishukuru serikali na Umoja wa Afrika Mashariki kwa kuridhia kujenga kituo kikubwa cha matibabu ya uloto na tafiti Afrika Mashariki na Kati. "Napenda kushukuru serikali yetu kwa kuridhia kituo cha umahiri cha upandikizaji uloto kujengwa BMH na kituo hiki kikikamlika kitasaidia kwenye matibabu ya wagonjwa wa selimundu na kufanya tafiti ambazo zitasaidia katika kugundua matibabu zaidi ya selimundu," ameendelea Prof. Makubi.

Kwa upande wake Dkt. Shakiru Jumanne ambae Amidi shule kuu ya Tiba katika chuo kikuu cha Dodoma (UDOM) na pia daktari bingwa wa magonjwa ya damu amesema kuwa UDOM itaendelea kuzalisha wataalamu na kufanya tafiti mbalimbali kwa ajili ya kupata matibabu ya ugonjwa huu.

"Chuo kikuu cha UDOM kinaendelea kuzalisha wataalamu ambao watasaidia katika kutoa huduma kwa wagonjwa wa selimundu lakini pia kufanya tafiti ili kugundua matibabu zaidi na namna ya kudhibiti ugonjwa huu," amesema dkt. Shakiru.

Everest Mayala ni mtoto mmoja wapo kati ya watoto 21 waliopandikizwa uloto ameishukuru serikali kwa uwekezaji huu mkubwa ambao umeletwa nchini.

"Naishukuru serikali yangu ya Tanzania kwa uwekezaji huu mkubwa ambao umeleta muarobaini wa ugonjwa wa selimundu nchini lakini naomba huduma hii ifikie watu wengi zaidi kwani watoto wengi wanateseka na ugonjwa huu," amesema Everest.

Kauli mbiu ya mwaka huu ya siku ya selimundu duniani ni; Hatua Madhubuti za Kitaifa kwa Matokeo Chanya ya Kijamii: Kuwezesha Jamii Kutambua, Kuzuia na Kukabiliana na Sikoseli.