BMH YAWAPOKEA MADAKTARI BINGWA WABOBEZI KUTOKA UHOLANZI KWA KUSHIRIKIANA NA TAASISI YA ZGT OVERZEE KUANZA KAMBI YA UPASUAJI WA MATUNDU MADOGO
Na Ludovick Kazoka na Gladys Lukindo, Dodoma: Aprili 13
Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kwa kushirikiana na Madaktari Bingwa Wabobezi kutoka shirika la afya la ZGT Overzee Foundation la nchini Uholanzi leo wameanza kambi ya pamoja ya Matibabu ya upasuaji wa Matundu (Laparascopic and Arthrospic Surgeries) itakayofanyika hadi Aprili 17, 2026.
Mapema leo wakati wa kupokea timu hiyo kutoka uholanzi, akimuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Prof Abel Makubi, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu wa BMH, Ndg Teophory Mbilinyi, amesema kambi hii itahusisha huduma mbalimbali za afya.
" Tunathamini sana uwepo wenu hapa kwa kuwa utawaongezea maarifa wataalamu wetu," amesema Ndg. Mbilinyi.
Ndg. Mbilinyi ametaja huduma zitakazotelew kwenye kambi hiyo ya pamoja ni pamoja na upasuaji kwa kutumia matundu madogo, matibabu ya kinamama, mfumo wa mkojo, upandikizaji figo, maumivu ya muda mrefu ya magoti na nyonga na uvimbe kwenye tumbo.
Kwa upande wake, Kiongozi wa msafara wa timu ya wataalamu kutoka Shirika la ZGT Overzee la Uholanzi, Bi. Joyce Rebergen, amefurahi kushirikiana na BMH.
"Kambi hii ya pamoja kati ya BMH na wataalamu wetu wa ZGT Overzee itasaidia kuwaongezea maarifa wenzetu wa BMH," alisisitiza Bi. Joyce.
Aidha, pande hizo mbili zilitumia fursa hiyo kukamilisha mchakato wa makubaliano ya mashirikiano kati ya pande hizo mbili.