WATOTO WENYE CHANGAMOTO ZA MOYO KUTOKA NCHINI BURUNDI WAANZA KUFANYIWA UPASUAJI BMH
Na Jeremia Mwakyoma & Jeremiah Mbwambo
Picha na Gladys Lukindo
DODOMA - JULAI 6, 2026
Daktari Bingwa Bobezi wa magonjwa ya moyo wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) John Meda amesema kuwa leo wameanza kuwafanyia upasuaji watoto wenye changamoto za moyo waliotoka nchini Burundi na kuwa upasuaji huo umekuwa wa mafanikio.
"Madaktari Bingwa Bobezi wa BMH tunashirikiana na Madaktari Bingwa Bobezi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), tuliwapokea watoto tangu Jumamosi na tulishawafanyia uchunguzi wa kina, leo tumeanza kuwafanyia upasuaji, tutaendelea hadi tutakapokamilisha kuwahudumia wote" alifafanua Dkt. Meda.
Dkt. Meda ameongeza kuwa kambi hii ya upasuaji wa moyo kwa watoto hao kutoka Burundi ni muendelezo wa kambi ambayo BMH ilifanya nchini Burundi mwaka 2025; Dkt. Meda anasema kuwa matatizo hayo ya moyo kwa watoto hao wamezaliwa nayo.
Dkt. Meda amesema kuwa kwa sasa uwekezaji uliofanywa na Serikali hapo BMH, unaiwezesha kuwa kituo cha kutoa matibabu ya ubobezi ya moyo kwa wananchi kutoka Mataifa ya jirani yanayotuzunguka kwa huduma za uchunguzi mishipa ya moyo, uzibuaji bila kufungua kifua, kuotesha mishipa, matundu kwenye moyo na upasuaji, umeme wa moyo, kupandikiza (betri) vianzisha mwendo kwenye moyo (pacemaker).
Awali asubuhi leo , Mkurugenzi Mtendaji BMH Prof Abel Makubi, alikutana na watoto hao wakiwa na wazazi wao, Mwambata wa Ubalozi wa Tanzania nchini Burundi ili kuwajulia hali zao na kuwatakia afya njema.