DIAMOND PLATNUM NA BAADHI YA WADAU WAKE WAICHANGIA BMH MIL 185 KUSAIDIA MATIBABU YA UPANDIKIZAJI ULOTO KWA WATOTO WA SICKLE CELL NA FIGO

Published: May 10, 2026
DIAMOND PLATNUM NA BAADHI YA WADAU WAKE WAICHANGIA BMH MIL 185 KUSAIDIA MATIBABU YA UPANDIKIZAJI ULOTO KWA WATOTO WA SICKLE CELL NA FIGO cover image

Na Jeremia Mwakyoma na Gladys Lukindo

Picha na Jeremiah Mbwambo

DODOMA - MEI 8, 2026

 

MSANII maarufu wa muziki wa kizazi kipya nchini, Diamond Platnumz, leo ametembelea Hospitali ya Rufani ya Benjamin Mkapa (BMH) jijini Dodoma na kuchangia fedha kiasi cha shilingi Milioni 185 kwa ajili ya kusaidia huduma za matibabu ya upandikizaji Uloto kwa Watoto wenye ugonjwa wa Selimundu na upandikizaji Figo kwa Wananchi wenye uhitaji.

 

Diamond amesema kuwa hatua hiyo ya kuchangia kiasi hiko cha fedha ni mwanzo tu wa mashirikiano na BMH na kuahidi atakuwa balozi wa kutangaza uwekezaji mkubwa uliofanyika katika BMH na kuongeza kuwa atawashirikisha Wadau wake anaoshirikiana nao katika kazi za sanaa na makampuni ya kibiashara katika kuunga mkono kuchangia huduma za Afya hapo BMH.

 

"Niipongeze Serikali chini ya Uongozi wa Mhe Rais Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa hapa BMH, pia watumishi wa BMH kwa moyo wa kujitoa, wito na kuhudumia wananchi; kwa mambo mazuri haya niliyoyaona hupa BMH, naahidi nitakuwa balozi wa kusaidia kufikisha elimu ya huduma za BMH na hata kushirikiana kutatua changamoto mbalimbali. Makampuni ya Wasafi na Washirika wetu tutaendelea kwa pamoja kushirikiana na BMH" alisisitiza Diamond.

 

"Tulizoea kusikia huduma hizi za kibingwa na kibobezi zinapatikana nje ya nchi na tunazifuata lakini leo huduma hizi zinatolewa hapahapa nchini watu wa mataifa ya nje ya tanzania wanakuja kuzifuata Tanzania katika Hospitali ya BMH kama upandikizaji uloto, upandikizaji figo, upasuaji moyo na mengine mengi" aliongeza Diamond.