JESHI LA POLISI MKOANI DODOMA LAISHUKURU BMH KWA KUWASOGEZEA HUDUMA KARIBU.
Na. Gladys Lukindo na Carine Senguji, Agosti 16 2025. DODOMA
Jeshi la Polisi mkoani Dodoma laishukuru Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kwa kuwasogezea huduma za uchunguzi wa magonjwa mbalimbali katika kituo cha afya cha Polisi.Â
Akizungumza mapema hii leo Kaimu Kamanda wa Polisi Dodoma, Kamishina Msaidizi wa Polisi, Mwamafupa William amesema kuwa wanaishukuru BMH kwa kuwasogezea huduma karibu kwa kuzingatia majukumu yao.
"Kipekee tunamshukuru Prof. Abel Makubi na uongozi mzima wa BMH kwa kusogeza huduma hizi kwa jeshi la Polisi pamoja na familia zao, huduma hizi zimekua za muhimu sana kwetu ukizingatia majukumu yetu ya kila siku ambapo hatupati muda wa kutosha kupima afya zetu," amesema kamanda Mwamafupa.
Kamanda Mwamafupa ameendelea kwa kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha kambi za madaktari bingwa wa Samia.
"Namshukuru sana Mhe. Rais kwa kuanzisha kambi za madaktari bingwa wa Samia kwa ajili ya wananchi na hii inaonesha jinsi gani Rais wetu anajali wananchi na hii imepelekea na sisi Jeshi la Polisi kupata huduma hizi katika kituo chetu hichi cha afya," ameendelea kamanda Mwamafupa.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma amewataka maaskari wote pamoja na familia zao kutumia fursa hii vizuri ili kujua afya zao.
"Niwaombe maaskari wote pamoja na familia zao kutuumia fursa hii ya kuangalia afya zao na kama watakua na matatizo wafanye matibabu mapema wasisubiri tatizo kuwa kubwa, mimi binafsi nimechunguza afya yangu na nipo vizuri, " ameongeza Kamanda Mwamafupa.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Kinywa na Maneno kutoka BMH, Josephat Lutale ameainisha huduma zinazotolewa na BMH kwenye kambi hiyo.
"Kwenye kambi hii BMH tumeleta huduma za magonjwa ya moyo, masikio, pua na koo, magonjwa ya macho, magonjwa ya kinywa na meno, magonjwa ya mifupa na magonjwa ya wanawake," amesema Dkt. Lutale.
 Dkt. Lutale amesema kuwa mpaka sasa wamefanikiwa kuona wagonjwa takribani 150 tokea kambi imeanza.
"Mpaka sasa tumeona watu 150 tokea tulipoanza kambii hii Jumanne na tumetoa rufaa kwa watu zaidi 100 kufika BMH kwa ajili ya matibabu zaidi," ameongeza Dkt. Lutale.
Dkt. Lutale amemalizia kwa kusema kuwa lengo la kambi hii ni kufikia askari wote mkoa wa Dodoma ili waweze kuwa na afya njema na kutekeleza majukumu yao kwa weredi