KAMBI YA MATIBABU YA UPASUAJI WA MASIKIO PUA NA KOO INAYOENDESHWA NA MADAKTARI BINGWA WA BMH KWA KUSHIRIKIANA NA MADAKTARI BINGWA KUTOKA UTURUKI YAZINDULIWA

Published: Dec 10, 2025
KAMBI YA MATIBABU YA UPASUAJI WA MASIKIO PUA NA KOO INAYOENDESHWA NA MADAKTARI BINGWA WA BMH KWA KUSHIRIKIANA NA MADAKTARI BINGWA KUTOKA UTURUKI YAZINDULIWA cover image

Na Jeremia Mwakyoma
DODOMA - DISEMBA 4, 2025

Akimuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya kuzindua kambi hiyo iliyoanza Disemba mosi na itakayokwenda hadi Disemba 7, 2025, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu wa Wizara ya Afya Bw. Issa Ng'imba amepongeza ushirikiano uliopo kati ya Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) na Shirika la Hands Giving Lives la nchini Uturuki uliofanikisha Kambi hiyo ya pamoja ya Upasuaji wa Masikio.

"Kambi hii imetoa fursa ya Wananchi kupata huduma za ubingwa bobezi wa upasuaji masikioΒ  ambapo jumla ya Wananchi 10 watafanyiwa upasuaji, lakini imetoa fursa ya kuwajengea uwezo zaidi Madaktari Bingwa wa BMH, Chuo kikuu cha Dodoma na madaktari Bingwa kutoka Hospitali za Rufaa za Mikoa ya Dodoma, Tabora na Manyara kupitia mafunzo ya upasuaji yaliyotolewa na Mabingwa Wabobezi kutoka Uturuki" alisisitiza Bw. Ng'imba.

Bw.Ng'imba ametoa rai kuongeza wigo wa ushirikiano kutoka matibabu ya Masikio, Pua na Koo badala yake kuongeza maeneo mengine zaidi ya matibabu yenye uhitaji na kuongeza idadi zaidi ya Mikoa itakayonufaika na mafunzo ya kujengewa uwezo.

Mkurugenzi Mtendaji wa BMH Prof. Abel Makubi pamoja na kushukuru, ametaja huduma hiyo ya Upasuaji wa Masikio (Temporal Bone Surgeries) itakayotolewa kwa Wagonjwa hao 10 kuwa ni moja ya operesheni ngumu ambazo kwa hapa nchini zilikuwa zikifanyika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili tu, tena kwa Madaktari wachache.

"Hivyo BMH itakuwa Hospitali ya pili hapa nchini kutoa huduma hiyo ya operesheni ya masikio inayohitaji utaalamu wa hali ya juu, vifaa vya kisasa na umakini mkubwa wa wataalamu, hivyo Wananchi wenye changamoto za kusikia na matatizo mengine ya masikio watambue kwa sasa Hospitali zetu zinatoa Matibabu ya Ubingwa wa Juu yatakayoweza kusaidia kutibu matatizo yao " alisisitiza Prof. Makubi.

Prof. Makubi alimaliza kwa kumshukuru Mhe Rais Samia Suluhu Hassan kwa kukuza mashirikiano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Uturuki kadhalika Wizra ya Afya, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Ubalozi wa Tanzania nchini Uturuki kwa kuratibu na kusimamia suala hili la ushirikiano lililoleta tija.

Aidha, kwa upande wake Rais wa Shirika la Hands Giving Lives la Uturuki na kiongozi wa Timu ya Madaktari Bingwa Wabobezi kutoka Uturuki Hatice Ozdemir amesema nchi ya Uturuki inapenda kushirikiana na Tanzania kwenye maeneo mengi na wao wanafurahi kupata nafasi ya kushirikiana na BMH kwa kuzingatia matibabu haya ya Upasuaji wa Masikio yanahitaji miundombinu na vifaa vya kisasa kama ilivyo BMH na amesema Shirika lake liko tayari kushirikiana na BMH kwenye maeneo mengine zaidi ya utoaji huduma.Β