MATUMIZI YA TIMU JUMUISHI ZA MATIBABU (MULTI DISCIPLINARY TEAMS - MDTs) YAPEWE MSISITIZO KUBORESHA ZAIDI HUDUMA KWA WAGONJWA
MATUMIZI YA TIMU JUMUISHI ZA MATIBABU (MULTI DISCIPLINARY TEAMS - MDTs) YAPEWE MSISITIZO KUBORESHA ZAIDI HUDUMA KWA WAGONJWA
Na Jeremia Mwakyoma
Picha na Gladys Lukindo
DODOMA - JAN 28, 2026
Uongozi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) umewasisitiza watumishi wake kuweka mkazo na kuziimarisha timu jumuishi za matibabu (MDTs) kwa kuzingatia kuwa timu hizo zikifanya kazi yake ipasavyo zinasaidia kuboresha kiwango cha huduma zinazotolewa kwa Wagonjwa kwa kuzingatia kuwa mwili wa binadamu ni muunganiko wa mifumo mingi (systems) ikiwemo mfumo wa chakula, wa kupumua na mifumo mingine hivyo mfumo mmoja ukipata hitilafu kuna uwezekano mkubwa wa mifumo mingine kuathirika.
Msisitizo huo umetolewa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa BMH Dkt. Henry Humba wakati wa kikao cha mafunzo kwa Watumishi wa BMH kilichoangazia manufaa ya kuziimarisha na kuzitumia timu jumuishi za matibabu.
"Wataalamu lazima tuzingatie kufanya kazi kama timu na kushirikishana katika kutoa matibabu kwa wagonjwa; mgonjwa anaweza kuja na matatizo zaidi ya moja au akaja na tatizo linaloweza kunsababishia matatizo mengine ya kiafya hivyo timu hizi zenye Wataalamu wenye taaluma mbalimbali kulingana na shida ya mgonjwa zitasaidia kumpatia matibabu bora na sahihi" alisisitiza Dkt. Humba.
Aliongeza kuwa suala la kuboresha ubora wa huduma za Afya BMH ni endelevu kila siku na ni sehemu ya misingi ya utamaduni wa BMH (BMH Culture) kwa kuzingatia BMH ni Hospitali kubwa na kimbilio la wananchi wengi wakiwa na imani na BMH.
Akiwasilisha mada katika Kikao hicho, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa BMH Dkt. Mugisha Nkoronko amesema kuwa timu jumuishi za matibabu zinaleta matokeo mazuri ya matibabu aliyopata mgonjwa, zinasaidia kushughulikia matatizo mengi ya mgonjwa kwa wakati mmoja ili kumuokolea muda na kumpunguzia gharama.
Dkt. Nkoronko aliongeza kuwa, timu hizo zenye mchanganyiko wa wajumbe wenye utaaluma wa aina mbalimbali zinasaidia kuhakikisha usalama wa Mgonjwa wakati wa matibabu, vilevile vinasaidia taasisi kukidhi mahitaji ya msingi ya kupata ithibati za kimataifa katika huduma za Afya.