MKUTANO WA KWANZA TANZANIA WA UPANDIKIZAJI VIUNGO KUWAKUTANISHA MADAKTARI BINGWA KUTOKA NDANI NA NJE YA TANZANIA
Na Jeremiah Mbwambo,Dodoma
MADAKTARI Bingwa na wataalam wa afya,kutoka ndani na nje ya nchi, wanatarajiwa kukutana leo jijini Dodoma kujadili sera, mipango na mikakati ya kuendeleza huduma za upandikizaji viungo, hususan figo na Uloto hapa nchini.
Wataalam hao,watakutana katika kongamano la kisayansi la kimataifa, lilioandaliwa na Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya afya hapa likiwa nchini.
Kongamano hilo litakalohusisha watu kutoka mataifa tofauti,ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 10 ya hospitali hiyo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2015 kwaajiliya utoaji huduma mbalimbaliza kitabibu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mkurugenzi Mtendaji wa BMH Profesa Abel Makubi amesema kuwa, kongamano hilo linalenga kuwakutanisha wataalamu, wabobezi na wadau wa afya ili kubadilishana uzoefu, ujuzi na kujadili mwelekeo wa huduma za upandikizaji viungo nchini na kanda ya Afrika.
Amesema,washiriki wa kimataifa wanatarajiwa kutoka nchi za Nigeria, Uganda, Afrika Kusini, Italia, India, Japan na Singapore, huku taasisi mbalimbali za ndani zitakazoshiriki ni Wizara ya Afya, Hospitali ya Taifa Muhimbili, hospitali za rufaa za kanda ambazo ni KCMC,Bugando pamoja na vyuo vikuu vya UDOM, CUHAS, MUHAS na Aga Khan.
Mbali na kongamano hilo,Profesa Makubi amesema maadhimisho ya miaka 10 ya BMH yamehusisha shughuli mbalimbali tangu Oktoba 13, 2025, zikiwemo kambi za matibabu bure, mihadhara ya umma, mikutano na wadau, mbio za marathon na harambee ya kusaidia mfuko wa upandikizaji uloto kwa watoto wenye ugonjwa wa selimundu pamoja na huduma za upandikizaji figo.
Amesema shughuli hizo zinatarajiwa kuhitimishwa Julai 15, 2026 kwa majumuisho mbalimbali ambayo yataainishwa katika kilele hicho.
Alifafanua zaidi ya kuwa kupitia kongamano hilo, wadau wanatarajia kufikia maazimio yatakayosaidia kuboresha huduma za upandikizaji viungo, kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa, pamoja na kuchangia katika uboreshaji wa sera na sheria za afya nchini.
Aidha,alisema kongamano hilo linatarajiwa kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa huduma za upandikizaji viungo na kuiweka Hospitali ya Benjamin Mkapa katika nafasi ya juu kama kituo cha umahiri katika tiba za kisasa barani Afrika.
Hata hivyo amewataka wataalamu, wadau, viongozi na wananchi kwa ujumla kushiriki na kufuatilia kongamano hilo muhimu kwa maendeleo ya sekta ya afya nchini.