SERIKALI KUGHARAMIA VIFAA TIBA KWA AJILI YA VITUO VYA UMAHIRI VYA TIBA SARATANI NA UPANDIKIZAJI FIGO KATIKA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA.

Published: Sep 15, 2025
SERIKALI KUGHARAMIA VIFAA TIBA KWA AJILI YA VITUO VYA UMAHIRI VYA TIBA SARATANI NA UPANDIKIZAJI FIGO KATIKA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA. cover image

Na Ludovick Kazoka
DODOMA - SEPTEMBA 3, 2025

Serikali imekubali kugharamia vifaatiba katika Kituo cha Mafunzo na Matibabu ya Saratani na katika kituo cha upandikizaji figo katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) ya jijini Dodoma.

Ahadi hiyo imetolewa na Makamu wa Rais, Dkt Philip Isdor  Mpango, leo wakati wa ziara yake ya kikazi hospitalini Benjamin Mkapa ambapo Makamu wa Rais aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa kituo  cha  Saratani na kuzindua kituo cha upandikizaji figo.


"Serikali imepokea ombi la fedha kiasi cha shilingi  Bilioni 13.3 kwa ajili ya vifaa tiba vya kutolea huduma kwenye kituo cha Saratani na shilingi Bilioni 2.3 kwa ajili ya vifaa tiba katika kituo cha upandikizaji figo katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, niwaahidi Serikali itayapatia kipaumbele maombi haya ili wananchi waweze kupata huduma bora " alisisitiza Makamu wa Rais.

Dkt. Mpango aliongeza kuwa mapinduzi makubwa na uwekezaji uliofanywa na serikali katika miundombinu, vifaa tiba vya kisasa, Wataalamu wabobezi na kuanzishwa kwa huduma za ubingwa wa juu  imesaidia kupunguza rufaa za Wagonjwa kwenda nje ya nchi na imevutia wananchi kwenye nchi zinazotuzunguka kutaka kuja kutibiwa hapa nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Prof Abel Makubi, amesema kuwa miradi hiyo miwili ina gharama ya shilingi Bilioni 30.4 kwa upande wa kituo cha Saratani na shilingi Bilioni 1.7 kwa upande wa kituo cha upandikizaji figo, fedha zilizogharamiwa na Serikali.

 Prof. Makubi ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka 10 tangu kuanzishwa kwa BMH huduma za Afya za ubingwa zinazotolewa zimefika 20 huku huduma za Ubingwa Bobezi zimefika  17.

Katibu Mkuu wa Wizara ya  Afya Dkt. Seif Shekalage amebainisha kuwa azma ya Mhe. Dkt.  Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuifanya Tanzania kuwa kituo cha tiba utalii na ndiyo maana  Hospitali ya Benjamin Mkapa inaweza kutoka na kwenda Burundi kutoa matibabu ambayo yamekuwa kivutio cha wananchi wa Burundi kuja hapa nchini kupata huduma za matibabu.