MHE. DEO MWANYIKA (MB): WANANCHI WANA IMANI NA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA
Published on June 05, 2025

Na Jeremia Mwakyoma, Picha na Jeremiah Mbwambo
BUNGENI DODOMA - JUNI 3, 2025
Mbunge wa Njombe Mjini Mhe. Deo Mwanyika ameipongeza Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) na kuitaka kuendelea kuboresha zaidi huduma zake za Afya kwa kutambua kuwa Wananchi kwenye mikoa ya Kanda ya Kati na Mikoa iliyo jirani na Kanda ya Kati wana imani kubwa na Hospitali hiyo.
Mhe. Mwanyika ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda Biashara na Kilimo ametoa pongezi hizo leo alipotembelea banda la BMH katika maonesho ya huduma za Afya yanayoendelea kufanyika Bungeni Jijini Dodoma wakati huu wa uwasilishaji wa bajeti ya Wizara ya Afya.
"Wananchi wa Mikoa ya Ukanda wa Kati na Mikoa ya jirani inayozunguka, wana imani kubwa na BMH, mmefanikiwa kuwajengea wananchi imani kutokana na huduma bora za Afya mnazowapa" alifafanua Mhe. Mwanyika.
Aliongeza kuwa ninapokuwa jimboni kwangu Njombe Mjini nakutana na wananchi, wapiga kura wangu ambao wanasema mategemeo yao katika huduma za Afya ni Hospitali ya Benjamin Mkapa na wengi wanasafiri kutoka kwenye mikoa ya jirani kuja BMH.