MABORESHO YA HUDUMA ZA MAABARA BMH YAMEPUNGUZA RUFAA ZA WAGONJWA KWENDA HOSPITALI NYINGINE NA NJE YA NCHI

Published: Oct 23, 2025
MABORESHO YA HUDUMA ZA MAABARA BMH YAMEPUNGUZA RUFAA ZA WAGONJWA KWENDA HOSPITALI NYINGINE NA NJE YA NCHI cover image
Na Jeremia Mwakyoma
Picha na Gladys Lukindo
DODOMA - OKT. 23, 2025
 
 
Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa BMH Dkt. Henry Humba katika kikao cha kufanya mapitio na tathimini ya utendaji kazi wa idara ya maabara ya Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kwa mwaka 2024/2025 huku akisisitiza viwango kwenye maabara hiyo yenye kutambulika ubora wake na kuthibitishwa na Ithibati ya Jumuiya ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADCAS).
 
"Maabara kwa sasa imeongeza wigo wa kutoa vipimo, inatoa vipimo kati ya 1800-2200(kutoka wastani wa vipimo 900 mwaka 2022/2023) kwa siku, hiyo imewezesha  wananchi wengi wanaofika kupata huduma BMH kuwa  na uhakika wa kupata vipimo vyao hapa hapa BMH na hivyo kupunguza rufaa za kwenda Hospitali nyingine  na nje ya nchi pia" alibainisha Dkt. Humba. Aidha Maabara hiyo imeboresha muda wa kusubiri majibu ya vipimo vingi vya Damu kutoka masaa 5-6 hadi masaa 2-4 . 
 
 
Aliongeza kusisitiza juu ya umuhimu wa kuzingatia viwango vya ubora wa huduma za Maabara kuwa ni jambo la msingi katika utoaji huduma bora za Afya katika vituo vyote vya kutolea huduma na kuahidi uongozi wa BMH kupitia uwezeshaji wa Serikali utaendelea kufanya  uwekezaji wa vifaa tiba vya kisasa na upatikanaji wa Wataalamu wenye sifa na ujuzi wa teknolojia za maabara zinazohitajika. 
 
Nae Mkurugenzi wa Huduma Shirikishi wa BMH (DCS) Dkt. Humphrey Sawira amesema kuwa Maabara ya BMH kwa sasa ina ithibati kutoka Shirika la SADCAS ambalo linatoa ithibati za kimataifa za maabara jambo ambalo linawezesha vipimo na majibu yake kutoka BMH kutambulika na kuweza kutumika kwenye vituo vya huduma katika nchi mbalimbali za Afrika na Mataifa ya nje ya Afrika. 
 
"Maabara ya BMH sasa inashiriki kwenye tafiti mbalimbali za Afya kwa kushirikia na Chuo Kikuu cha Dodoma na vyuo vingine, inatumika pia katika kutoa mafunzo kwa Wataalamu wa Afya eneo la maabara" aliongeza Dkt. Sawira. 
 
Kwa upande wake Meneja wa Maabara BMH Farida Mbula amesema kuwa kwa mwaka 2024/2025 utekelezaji wa malengo  yaliyowekwa ulifanyika kwa asilimia 118.43% na sasa wanajipanga kuongeza wigo wa ushirikiano na maabara za maeneo mengine ili kuweza kuwapa huduma ya vipimo ambavyo havipatikani kwenye maabara hizo, huku wakiendelea kuboresha huduma kwa wateja na mawasiliano .
 
Kikao hiko cha kufanya mapitio na tathimini ya utendaji wa idara ya maabara BMH kwa mwaka mzima, kimeshirikisha pia Wadau wa nje ya BMH kama Bohari ya Dawa (MSD), Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Hospitali ya Rufaa ya Mkoa (DRRH), Idara ya Afya Halmashauri ya Jiji la Dodoma na CDC.