SHIRIKA LA KIMATAIFA LA NGUVU ZA ATOMIKI NA WHO WAFANYA TATHIMINI YA HUDUMA ZA MATIBABU YA SARATANI KATIKA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA.

Published: Sep 30, 2025
SHIRIKA LA KIMATAIFA LA NGUVU ZA ATOMIKI NA WHO WAFANYA TATHIMINI YA HUDUMA ZA MATIBABU YA SARATANI KATIKA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA. cover image

Na Jeremia Mwakyoma
Picha na Carine Senguji na Gladys Lukindo
DODOMA - SEPT. 23, 2025 

Timu ya Wataalamu kutoka Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki (IAEA) na  Shirika la Afya Duniani (WHO) na leo wametembelea Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) na kufanya tathimini ya huduma za matibabu ya Saratatani na kuridhishwa na uwekezaji unaofanyika Hospitalini hapo kwa ajili ya kutoa huduma ya matibabu ya Ugonjwa wa Saratani. 

"kupitia mradi wa IMPACT, umepata fursa ya kutathimini na kujionea huduma za matibabu ya saratani zinazotolewa na BMH, tumetembelea mradi wa ujenzi wa kituo cha mafunzo na matibabu ya Saratani kinachoendelea kujengwa, ziara hii ni sehemu ya Programu ya tathmini ya kina ya mahitaji ya nchi katika kukabiliana na ugonjwa wa saratani" alibainisha Kiongozi wa timu hiyo Dkt. Alfred Karagu ambae ni Mratibu wa programu ya Mapitio kutoka Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki (IAEA). 

Aliongeza kuwa tathmini kama hii ilifanyika mwaka 2006 na kupelekea kupatikana kwa mkakati wa taifa wa kudhibiti saratani ( National Cancer Control Stratergy ) ambao umefikia ukomo mwaka 2022 na sasa tunafanya mapitio kwa lengo la kushirikiana kuunda mkakati mpya wa Kitaifa. 

"Hongereni kwa kuwa na Hospitali ya kisasa, tumeona jitihada kubwa za ujenzi wa kituo cha Mafunzo na Matibabu ya Saratani, tunaimani kikikamilika kitawezesha kutoa huduma za matibabu ya Mionzi kwa Magonjwa ya Saratani na kuongeza uwezo wa nchi ya Tanzania katika kudhibiti na kutoa huduma za matibabu ya Saratani"  alisisitiza Dkt Alfred Karagu.


Prof Hanan Gewefel ambae ni mtaalamu wa radiolojia na tiba nyuklia kutoka IAEA alitoa wito kwa Wadau wa mapambano ya Saratani kuongeza nguvu katika utoaji elimu ya magonjwa ya Saratani na kuhamasisha Wananchi kuwa na utamaduni wa kufanya uchunguzi wa magonjwa ya saratani mara kwa mara hususani Saratani ya matiti kwa wanawake ambapo amejionea mashine ya kisasa ya Mammography inayotumika kugundua saratani ya matiti katika hatua za awali na hivyo kupunguza madhara ya saratani na gharama zinazoletwa kwa kuchelwa kupata matibabu. 

Nae Mratibu wa Saratani wa Taifa kutoka Wizara ya Afya Dkt. Caroline Mrema ameelezea kuwa ziara ya Timu ya WHO na IAEA inafanyika kwa mara ya pili sasa hapa nchini ambapo mara ya kwanza ilifanyika 2006 na tathimini ya uwezo wa  kudhibiti Saratani  iliyofanyika ilisaidia kupatikana kwa Makakati wa Taifa wa Kudhibiti Saratani nchini uliofika ukomo mwaka 2022 , na  katika tathimini hii ya mara ya pili inayofanyika wakati huu itatuwezesha kushirikiana na wadau kuhuisha na kuunda mkakati mpya wa kudhibiti saratani. 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa BMH Prof. Abel Makubi ameuelezea ujumbe huo kuwa, kwa sasa BMH inatoa huduma ya tiba kemia  (chemotherapy) na tiba shufaa (palliative) ya matibabu ya Saratani na inajiandaa kuingia katika kutoa tiba Mionzi (Radiotherapy) na Tiba Nyuklia (Nuclear Medicine)  kituo kitakapokamilika. 

"Serikali imetoa zaidi ya Shilingi Bil. 30 kujenga Kituo hiko, ambacho kitakuwa kikubwa hapa nchini na kitasaidia sana mafunzo na matibabu ya Saratani hapa nchini  na nchi za ukanda wa Africa mashariki na kati" aliongeza Prof Makubi na kuliomba shirika hilo kusaidia upatiakaji wa vifaa vya mradi wa tiba ya saratani na mafunzo zaidi kwa watalaamu wa mionzi. 

Mkuu wa Idara ya Saratani wa BMH Dkt. Jesse Kashabano amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa idara ya Saratani hapo BMH, tayari wameshahudumia Wagonjwa zaidi ya 15,000 huku wengi wao wakiwa wagonjwa wa Saratani ya Matiti ikifuatiwa na Tezi dume na aina nyingine za saratani, changamoto iliyopo mpaka sasa ni kukosekana kwa tiba mionzi ambapo taklibani asilimia 70 ya saratani huitaji mionzi ili kukamilisha matibabu. 

Dr. Kashabano alisisitiza kua kuelekea kukamilika kwa mradi wa kituo cha mafunzo na matibabu ya saratani, BMH inahitaji taklibani Tsh Billioni 13 ili kuweza kununua baadhi ya vifaa vya kutolea huduma katika kituo hicho.