MAADHIMISHO YA SIKU YA WAUGUZI DUNIANI BMH YAFANA, WAUGUZI WAASWA KUCHANGAMKIA FURSA ZA MASOMO NA KUJIENDELEZA KIELIMU

Published: Jul 04, 2026
MAADHIMISHO YA SIKU YA WAUGUZI DUNIANI BMH YAFANA, WAUGUZI WAASWA KUCHANGAMKIA FURSA ZA MASOMO NA KUJIENDELEZA KIELIMU cover image

Na Jeremia Mwakyoma na Jeremia Mbwambo


DODOMA - MEI 29, 2026



Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) leo imesherehekea maadhimisho ya siku ya wauguzi huku wauguzi wa BMH wakiaswa kuchangamkia fursa za masomo na kujiendeleza kielimu.

Akizungumza na Wauguzi wa BMH wakati wa maadhimisho hayo, Muuguzi Mkuu wa Serikali Ziada Sellah amewasisitiza Wauguzi pamoja na kujiendeleza kimasomo, wajitoe kushiriki katika kufanya tafiti mbalimbali za Afya ili kuendelea kuisaidia zaidi jamii.


"Napenda kutambua mchango wenu mkubwa Wauguzi wa BMH na Wauguzi wa maeneo mengine nchini kwa kuwahudumia Watanzania, nitoe wito kwenu muwe mstari wa mbele kutafuta na kuchangamkia fursa za mafunzo, Wizara pia itakuwa inawaletea fursa kila zitakapokuwa zikijitokeza kwa upande wa kozi zilizopo hapa nchini na hata ambazo hapa nchini hazipo Wauguzi ombeni na mtakapofuata taratibu vizuri Wizara itawaunga mkono"


Bi. Sella aliongeza kuwa, katika hatua za kuendelea kuboresha muundo wa kiutumishi kwa kada ya Wauguzi Wizara imeandaa mapendekezo ya kuwa na madaraja matano kuanzia Muuguzi Msaidizi (Certificate), Muuguzi (Diploma), Afisa Muuguzi (Bachelor Degree), Muuguzi Bingwa (Masters Degree) na Muuguzi Mshauri (PhD) na kuwa maslahi yatazingatia madaraja hayo.

"Mapendekezo hayo yameshaandaliwa, Wizara inasubiri kwenda kuyawasilisha katika baraza la Wizara ya nchi Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala bora, hivyo niwaombe tuendelee kujitoa kuwahudumia Wananchi tukizingatia miongozo na maadili ya taaluma za uuguzi" alisisitiza Bi. Sella.


Nae Mkurugenzi Mtendaji wa BMH Prof. Abel Makubi ametumia nafasi hiyo kuwapongeza Wauguzi wa BMH kwa kuwa wamekuwa nguzo kubwa sana katika kuboresha huduma za Afya Hospitalini hapo, huku akibainisha kuwa Wauguzi ndio wanakuwa na Wagonjwa kwa muda mrefu kuliko watumishi wa Afya wa Kada nyingine; Prof Makubi ameiomba Wizara iwape wauguzi wa BMH kipaumbele cha kupata nafasi za kwenda masomoni na kupata ufadhili.



Mkurugenzi wa Uuguzi wa BMH Bi. Mwanaidi Makao amesema kuwa kutokana na ukuaji wa BMH na upanuzi wa huduma zake, uongozi umekuwa ukiwapa Wauguzi wake fursa za kupata mafunzo ndani na nje na kuifanya BMH kuwa Hospitali inayotoa huduma za kisasa kiwango cha juu nchini.